TAFIRI NA FETA ZAAGIZWA KUZALISHA VIFARANGA MILIONI 10 VYA SAMAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.  Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA)  kufanya utafiti na kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki milioni 5 kila mmoja  kwa mwezi ili kupunguza changamoto ya gharama kubwa ya upatikanaji wa vifaranga  kwa wafugaji wa samaki.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo  Agosti 15, 2026 wakati wa ziara yake mkoani Mwanza ambapo pia amewataka wawekezaji wakubwa katika sekta ya ufugaji samaki kuongeza uzalishaji wao ili kuwa na mchango mkubwa na kuleta ushindaji katika sekta hiyo 

"Wawekezaji wakubwa katika ufugaji wa samaki lazima ukubwa wao katika uzalishaji watofautiane na wale wadogo. sitatoa kibali kwa wawekezaji wakubwa wanaofuga samaki wa mboga kama wafugaji wadogo wa samaki" alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Katika hatua nyingine Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameiagiza TAFIRI kufanya utafiti utakaosaidia kidhibiti na kulinda mazingira na fukwe za Ziwa Victoria ambapo ameitaka taasisi hiyo kishirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza ili kutathmini na kuja na suluhisho la kulilinda ziwa hilo ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa sheria.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema kupitia programu ya utoaji wa mikopo halmashauri, Wilaya hiyo imetoa zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana kufuga samaki kwa njia ya vizimba hatua ambayo imeongeza hamasa na mwamko wa ufugaji wa samaki katika wilaya hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Katikati) akikagua maabara inayotumiwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania kufanyia utafiti wa sekta ya uvuvi, wakati wa ziara yake mkoani Mwanza Agosti 15, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akikagua chakula cha samaki kinachotengezwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) wakati wa Ziara yake mkoani Mwanza Agosti 15, 2026

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi akimweleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa hatua waliyofikia Halmashauri ya Nyamagana katika uwezeshaji mikopo kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa vizimba, wakati wa ziara ya waziri mkoani Mwanza, Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania Dkt. Ismael Kimirei.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI