MKUU WA MKOA WA NJOMBE ATEMBELEA BANDA LA FETA KATIKA TAMASHA LA KIZIMKAZI

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Anthony John Mtaka, ametembelea Banda la Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) katika Tamasha la Kizimkazi, ambapo amejionea bunifu na teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta ya Uvuvi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

Bw. Mtaka akiwa bandani hapo 13 Agosti, 2026 ameipongeza FETA kwa ubunifu huo na kuitaka kusambaza na kutangaza teknolojia hizo nchi nzima, ili wananchi wengi zaidi wanufaike kwa kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao ya uvuvi, ajira na kipato.

 “Nchi nzima inahitaji uelewa na ujuzi kuhusu teknolojia hizi muhimu zinazobuniwa na Taasisi za Serikali. Hii itachochea maendeleo kwa wananchi wetu kupitia Sekta ya Uvuvi,” alisema Bw. Mtaka.

Aidha, ameitaka FETA kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia hizo kwa wadau na jamii ili kuimarisha usalama wa chakula, ajira, kipato na pato la Taifa. 

Naye Mkufunzi wa FETA Bw. Mashaka Kapagalla alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa FETA inaendelea kuzitangaza teknolojia hizo ili wananchi wazidi kufaidika na fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu, Pia   alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa FETA itaendelea kubuni teknolojia mpya ili kuongeza tija na uchangiaji wa Sekta ya Uvuvi katika pato la Taifa.

Teknolojia za FETA zinazooneshwa katika Tamasha hilo ni dema la kidigitali lililofungwa king'amuzi maalum kinachotoa taarifa samaki wakiingia mtegoni, teknolojia za kukaushia mazao ya samaki na mwani kwa kutumia nishati ya jua, gesi na umeme pamoja na utengenezaji wa maua ya mapambo kwa kutumia magamba ya samaki.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI