BANDARI ALIYOAHIDI MHE. DKT. SAMIA SASA IPO TAYARI – MHE. TELACK

Na Kilwa, Lindi

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, amesema Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, ambayo iliahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo tayari kuanza kutoa huduma baada ya kufikia hatua za mwisho za ukamilishaji wake.

Akizungumza leo Juni 25, 2026, wilayani Kilwa mkoani Lindi wakati wa zoezi la kihistoria la majaribio ya mitambo na miundombinu mbalimbali ya bandari hiyo, Mhe. Telack amesema kiwango cha ukamilishaji wa mradi huo kimefikia asilimia 99.99, huku hatua iliyobaki ikiwa ni kuwasha na kuthibitisha utendaji wa mitambo mbalimbali.

Amesema miongoni mwa majaribio yaliyofanyika leo ni pamoja na kuwasha mitambo  ya kuzalisha barafu, ambayo inauwezo wa kuzalisha barafu tani 100 kwa siku mitambo hiyo inauwezo wa kugandisha barafu kwa nyuzi joto 3 sentigredi.

“Hii ni ishara kuwa Bandari yetu sasa iko tayari kuanza kazi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika historia kwa kujenga Bandari ya kwanza ya kisasa ya uvuvi nchini, ambayo itafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi,” amesema Mhe. Telack.

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea kwa vitendo utendaji na ubora wa mitambo pamoja na miundombinu iliyojengwa katika bandari hiyo, mitambo iliyofanyiwa majaribio ni pamoja na mitambo ya kuzalisha barafu, mitungi ya kuhifadhia mafuta na vifaa vingine muhimu vitakavyotumika katika shughuli za bandari.

Mhe. Telack amesema ameridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika pamoja na ufanisi wa mitambo iliyowekwa, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 280 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uongozi wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, kwa usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mradi huo hadi kufikia hatua ya mwisho ya ukamilishaji wake.

Mhe. Telack pia amewahimiza wavuvi na wadau wote wa sekta ya uvuvi kuanza kujipanga kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa bandari hiyo ya kisasa, akieleza kuwa mradi huo utarahisisha shughuli za uvuvi, uhifadhi na biashara ya mazao ya uvuvi katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amesema Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ni miongoni mwa miradi muhimu inayolenga kuongeza uzalishaji, uchakataji na thamani ya mazao ya uvuvi nchini.

Amefafanua kuwa lengo kuu la ujenzi wa bandari hiyo ni kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa kuwezesha uhifadhi bora, uchakataji wa kisasa na upatikanaji wa masoko yenye tija zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Miundombinu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi George Kwandu, amesema matokeo ya majaribio yanaonesha kuwa mitambo yote inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kukidhi viwango vilivyokusudiwa.

Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya Majaribio ya Mitambo na Miundombinu mbalimbali ya Bandari hiyo, kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (wa pili kulia), akikagua ubora wa Barafu na Mtambo wa kuzalisha Barafu kwenye chumba cha kuzalisha barafu, wakati wa zoezi la kihistoria la majaribio ya Mitambo na Miundombinu mbalimbali katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, Juni 25, 2026 Kilwa - Lindi, wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohamed Sheikh.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (wa nne kulia), akikagua ubora wa Mtambo wa kusafisha na kuchakata bidhaa za Uvuvi, wakati wa zoezi la kihistoria la majaribio ya Mitambo na Miundombinu mbalimbali katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, Juni 25, 2026 Kilwa - Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (aliyeshikilia kitufe cha Mtambo wa Umeme), akikagua ubora wa Miundombinu hiyo, wakati wa zoezi la kihistoria la majaribio ya Mitambo na Miundombinu mbalimbali katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, Juni 25, 2026 Kilwa - Lindi, wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena.

Wadau mbalimbali wa Sekta ya Uvuvi pamoja na Viongozi wa Serikali, wakishuhudia jinsi miundombinu ya kamera za Ulinzi na Mawasiliano (CCTV Camera) zinavyofanya kazi, wakati wa zoezi la kihistoria la majaribio ya Mitambo na Miundombinu mbalimbali katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, Juni 25, 2026 Kilwa - Lindi.














Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI