Nav bar

Alhamisi, 24 Agosti 2023

VIJANA BBT MIFUGO WAUZA MIFUGO YAO

Vijana waliojiunga na programu ya BBT Mifugo wanaoendelea na mafunzo ya unenepeshaji katika kituo cha Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kikulula wameonja matunda ya mafunzo hayo baada ya kuuza ng'ombe 310 waliowanenepesha kwa muda wa miezi mitatu.


Hayo yalifahamika wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliyoifanya katika kituo hicho kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera Julai 21, 2023.


Akiongea kwa niaba ya vijana wenzake, Salum Husidicheki alisema mpaka sasa wameshauza ng'ombe 310 ambapo awamu ya kwanza waliuza ng'ombe 150 na awamu ya pili wameuza ng'ombe 160.


"Wastani wa bei tulizofanikiwa kuuza ng'ombe wetu sio chini ya Laki sita na nusu (650,000) na katika mauzo hayo faida kwa kila ng'ombe haipungui Elfu tisini (90,000)," alisema




Alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata fursa hiyo ya mafunzo wao kama vijana wa kitanzania kwani wanaamini kupitia mafunzo hayo wataweza kuwa na ujuzi wa ufugaji wa kibiashara na kukuza kipato chao.


Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliwapongeza vijana hao kwa hatua hiyo ya kuanza kuuza mifugo kwani inaashiria kuwa tayari wameshaanza kupata ujuzi ambapo watakapomaliza mafunzo yao wanaweza kuendesha maisha yao kupitia biashara hiyo ya mifugo.


Alisema maono na dira ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuifanya hiyo programu ya bbt inaenea nchi nzima na vijana waingie katika uzalishaji wa mali kupitia rasilimali zilizopo hapa nchini.


"Tunataka nyie muwe mabalozi wa mabadiliko katika sekta ya mifugo kwa kwenda kutekeleza yale ambayo mmejifunza katika programu hii ili itusaidie kupata wafanyabiashara wengi wa mifugo nchini," alisema

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni