Katika kutambua juhudi za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendeleza na kuinua vijana kupitia programu ya BBT, Kampuni ya vijana wazawa hapa nchini ya JEAA VITAGRO imeamua kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa Tani mbili (2) za chakula cha mifugo (silage) pamoja na mifuko kumi (10) ya kilo mbili ya madini maalum ya kunenepesha mifugo ili wapewe vijana kwa ajili ya kulisha mifugo yao.
Hayo yalifahamika wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliyoifanya kwenye Kampuni hiyo iliyopo Wilayani Misenyi, Mkoani Kagera Julai 22, 2023.
Wakati akiwasilisha taarifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JEAA VETAGRO Solution LTD, Adam Owange alimwambia Waziri Ulega kuwa wanaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya uzalishaji wa malisho kibiashara.
"Mhe. Waziri kwa kutambua juhudi za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendeleza na kuinua vijana kupitia programu ya BBT Mifugo, na kwa sababu sisi tunazalisha malisho kibiashara, tunapenda kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa Tani mbili za chakula cha mifugo (silage) pamoja na mifuko kumi ya kilo mbili ya madini maalum ya kunenepesha mifugo ili wapelekewe vijana kwa ajili ya kunenepesha mifugo yao," alisema
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliupongeza uongozi wa kampuni hiyo akisema kuwa shughuli wanayofanya ya uzalishaji wa malisho ya mifugo kibiashara ni miongoni mwa hatua muhimu katika kuleta mapinduzi ya uzalishaji wa maziwa mengi mkoani Kagera na nchi nzima kwa ujumla.
Aliendelea kusema kuwa shughuli wanayoifanya Kampuni hiyo ya JEAA VITAGRO Inaisaidie Serikali kuondokana na kero za migogoro ya kila uchao baina ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.
Aidha, Waziri Ulega kwa kutambua kazi hiyo nzuri wanayoifanya ya kuzalisha malisho bora kwa ajili ya ng'ombe wa maziwa na nyama, aliwahakikishia kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuwaunga mkono ili waweze kuwa chachu ya mapinduzi ya ufugaji wa kisasa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni