Nav bar

Jumanne, 18 Aprili 2023

WAFUGAJI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA WAKATI WA USAFIRISHAJI WA MIFUGO

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde amewataka wafugaji kuzingatia sheria wakati wa usafirishaji wa mifugo kutoka wilaya moja kwenda nyingine.

 

Naibu Waziri Silinde ameyasema hayo leo (18.04.2023) bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Naghenjwa Kaboyoko aliyeuliza kuhusu katazo la kisheria la kuswaga mifugo ili kuzuia uharibifu wa mazingira.


Naibu Waziri Silinde amesema kuwa usafirishaji wa mifugo hufanyika chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama, Sura 156, na Kanuni zake za Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao ya Wanyama, GN 28 za mwaka 2007, ambapo usafirishaji wa mifugo kutoka wilaya moja kwenda nyingine hufanyika baada ya mifugo kukaguliwa na wataalamu na kupatiwa kibali cha kusafirishwa.  Aidha, Waraka wa Rais Na. 1 wa Mwaka 2002 uliziagiza Serikali za Mitaa kote nchini kutunga Sheria ndogo ili kuzuia uswagaji wa mifugo.

 

Vilevile Naibu Waziri Silinde amesema kuwa sheria hiyo ipo, hivyo wafugaji wanahimizwa kuzingatia Sheria ya Magonjwa ya Wanyama, Sura 156 pamoja na Sheria ndogo zilizopo ndani ya Halmashauri zao zinazozuia uswagaji wa mifugo. Pia amezielekeza Halmashauri ambazo mpaka sasa hazijatunga Sheria ndogo za kuzuia uswagaji wa mifugo zifanye hivyo mara moja.

 

Aidha, akijibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Naghenjwa Kaboyoko aliyeuliza kama serikali ilitoa maelekezo kwa halmashauri za wilaya kuhusu kutenga maeneo kwa ajili ya kufugia, na kuhusu kutumika kwa Ranchi za Taifa kutumika kutoa elimu kwa wafugaji wakubwa ili wafuge kisasa na sio kutegemea kuswaga/kuchunga, ambapo Naibu Waziri Silinde amesema kuwa serikali kwa kuanzia tayari imeshatenga hekta milioni 3.38 kupitia kwenye serikali za vijiji kwa ajili ya kufugia lakini pia serikali imeweka mkakati wa kutumia Ranchi za Taifa kama mashamba darasa kwa wafugaji hapa nchini.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni