Nav bar

Jumatatu, 17 Aprili 2023

MWAMBA DARASA UMEONGEZA UZALISHAJI WA PWEZA-SILINDE

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango wa mwamba darasa uzalishaji wa Pweza umeongezeka ambapo mwaka 2017 uzalishaji eneo la Songosongo ulikuwa tani 9.8 lakini baada ya ufungaji wa hiyari wa uvuvi wa zao hilo  uzalishaji uliongezeka hadi tani  37.6 mwaka 2019 zenye thamani ya shilingi milioni 373.5.


Mhe. Silinde amebainisha hayo wakati wa halfa ya uzinduzi wa mwongozo wa usimamizi wa ufungaji wa  hiyari wa uvuvi wa Pweza (Mwamba darasa) iliyofanyika leo Aprili 15, 2023  Bagamoyo mkoani Pwani.


"Ongezeko hili la uzalishaji limesababisha kuongezeka kwa ongezeko la upatikanaji wa malighafi kwenye viwanda vyetu nchini, mfano nimearifiwa kuwa kiwanda cha Alfa kimeongeza uzalishaji kutoka kilo 213,945 mwaka 2020 mpaka kilo 587400 mwaka 2022" Ameongeza Mhe. Silinde.


Aidha Mhe. Silinde amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa zao la Pweza linachukua nafasi ya pili baada ya mazao ya Sangara na ni la kwanza kwa upande wa mazao ya bahari ambapo mauzo yake nje ya nchi kwa mwaka 2022 yalifikia kiasi cha tani 1056 ambao waliuzwa kwa thamani ya shilingi bilioni 19.8.


Akizungumzia mchango wa zao hilo la uvuvi kwa mwananchi mmoja mmoja Mhe. Silinde amesema kuwa tofauti na mazao mengine Uvuvi wa Pweza unahusisha jinsia zote huku wastani wa kipato ukiwa ni shilingi 100,000 kwa mvuvi wakati wa ufunguzi wa msimu.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la kuhifadhi uhai asili (WWF) Bi. Metrida Semfukwe amesema kuwa mwongozo huo  utaendelea kuutambulisha kimataifa uvuvi wa Pweza unaofanyika hapa nchini.


"Ufungaji huu wa miamba ya Pweza kwa hiyari unawapa fursa wavuvi kuamua wenyewe wakati muafaka wa kufunga, nani wa kulinda miamba yao, upangaji wa bei na mgawanyo wa mapato wanayoyapata kutokana na uvuvi na hii ni hatua kubwa sana kwa jamii kusimamia kumiliki rasilimali zao kwa dhati" Amesema Bi. Semfukwe.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Bw.  Shauri Selenda amesema kuwa takribani asilimia 14 ya mapato ya Halmashauri hiyo yanatokana na uuzaji wa mazao ya uvuvi ikiwemo Pweza hivyo anaamini kadri mazao hayo yanavyoongezewa thamani na mapato ya Halmashauri yake yanaongezeka.


Mwongozo huo wa usimamizi wa ufungaji wa  hiyari wa uvuvi wa Pweza (Mwamba darasa) uliozinduliwa leo una sura 5 ambazo zinaainisha taratibu za kufuatwa na wahusika wakati wa ufungaji huo wa hiyari wa muda wa miamba usiozidi miezi 3.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akiwalisha samaki chakula muda mfupi baada ya kufika kwenye mabwawa ya kufugia samaki aina ya "Tilapia" yanayomilikiwa na kampuni ya TANLAPIA iliyopo Wilayani Bagamoyo Aprili 15, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akimuangalia samaki aina ya "kingfish" aliyemkuta kwenye soko la samaki la Bagamoyo Aprili 15,2023 ambako alifika kwa ajili ya kukagua namna biashara za Uvuvi zinavyofanyika sokoni hapo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ( katikati) akizindua mwongozo wa usimamizi wa ufungaji wa  hiyari wa uvuvi wa Pweza (Mwamba darasa) kwenye hafla fupi iliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani, Aprili 15, 2023. Kulia ni Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la kuhifadhi uhai asili (WWF) Bi. Metrida Semfukwe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni