Nav bar

Jumatatu, 17 Aprili 2023

​ULEGA: VITUO ATAMIZI FURSA YA AJIRA KWA VIJANA

Na Mbaraka Kambona


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara yake imeanzisha vituo atamizi vya kuwafundisha vijana ufugaji wa kisasa wa mifugo na samaki lengo likiwa ni kujibu changamoto ya ajira kwa vijana iliyopo hapa nchini.


Waziri Ulega aliyasema hayo katika Kongamano la Tisa la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu maswala ya sera linalofanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2023.


“Tunamshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuanzisha programu hii kwa ajili ya kuandaa vijana kufanya ufugaji wa kibiashara ambapo kwa mwaka huu tumeanzisha vituo atamizi nane (8) vya kuwafundisha vijana ufugaji kwa tija”, alisema



Alisema kuwa kila mwaka takriban vijana 1600 wanahitimu ngazi mbalimbali za elimu katika vyuo vya mifugo na kati ya hao 150 tu ndio hupata nafasi katika mfumo rasmi wa ajira hivyo lengo la ubunifu huo walioufanya ni kuwezesha vijana wanaobaki nje ya mfumo rasmi wa ajira kujiajiri kupitia unenepeshaji na uuzaji wa mifugo yao ndani na nje ya nchi.


“Mipango yetu katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ni kuwa na vituo atamizi 30 ambavyo vitakuwa na vijana wasiopungua 30 na kutufanya kuwa na vijana 900 ambao watakuwa wamepata mafunzo na hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira hapa nchini ”,alifafanua


Aliongeza kuwa tayari wizara imeshatafuta masoko kwa ajili ya vijana hao kuuza mifugo yao ambapo kwa mwaka vijana hao watauza mifugo yao takriban mara nne kwa mwaka na hivyo kuwawezesha kupata kipato ambacho kitawasaidia kujiajiri baada ya kumaliza mafunzo.


Halikadhalika, aliongeza kuwa vituo atamizi hivyo wamevianzisha pia kwa upande wa sekta ya uvuvi kwa ajili ya vijana kuboresha ujuzi wa ufugaji wa samaki na uvuvi.


Kauli mbiu na dhima ya Kongamano hilo ni “Ushindani wa Tanzania Katika Soko Huru Barani Afrika (AfCFTA): Changamoto na Fursa Katika Sekta ya Kilimo, Mifugi na Uvuvi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni