Nav bar

Jumamosi, 1 Aprili 2023

SEKTA BINAFSI YASHIRIKI ZAIDI UCHUMI WA TAIFA KWA UFUGAJI WA KUKU

Na. Edward Kondela


Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa sekta binafsi kushiriki katika mnyororo wa ukuzaji uchumi wa taifa ambapo takriban kaya milioni nne zinajihusisha moja kwa moja na ufugaji wa kuku.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ameeleza hayo (22.03.2023) jijini Dodoma wakati wa kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichohusisha baadhi ya wazalishaji wa vifaranga na wafugaji wakubwa kuangalia namna bora yao wao kufanya biashara na kukuza ajira.


Prof. Shemdoe amesema katika kikao hicho ambacho kimetoka na maazimio yasiyopungua tisa kuangalia namna bora yao wao kwa wao kufanya biashara na kuchangia katika pato la taifa ni muhimu kukaa pamoja na kukubaliana na mambo kadhaa ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kujenga mazingira bora ya kufanya biashara.


“Tunashukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha sekta binafsi zinachangia katika mnyororo wa ukuzaji uchumi wa taifa leo kumekuwa na muunganiko wa wazalishaji wa vifaranga vya kuku na wafugaji wanakaa pamoja na kukubaliana mambo kadhaa ya kufanyia kazi ili kukuza tasnia ya kuku.” Amesema Prof. Shemdoe


Ameongeza kuwa maazimio yaliyofikiwa yataweza kukuza tasnia ya kuku ambayo ni muhimu kwa kaya takriban milioni nne ambazo zimejiajiri moja kwa moja katika tasnia hiyo na kwamba watu wengi zaidi wanahusika katika mnyororo wa thamani kwa kuwa asilimia kubwa ya mazao ya kuku kwa maana ya nyama na mayai yana soko kubwa ndani na nje ya nchi.


Aidha, amebainisha kuwa tasnia ya kuku, ng’ombe na nyingine za Sekta ya Uvuvi zinapaswa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.


Katika kikao hicho ambacho wadau mbalimbali wametoa maoni yao juu ya changamoto wanazopata ikiwemo ya uhaba na ubora wa vifaranga vinavyozalishwa pamoja na uhaba wa nafaka za kutengenezea vyakula vya kuku, Prof. Shemdoe amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imechukua maoni ya namna wadau wanavyoiomba wizara iweke mkono wake zaidi ili kuhakikisha upatikanaji wa vifaranga bora kwa bei nafuu pamoja na nafaka za kutengenezea vyakula vya kuku ili kupunguza gharama.


Nao baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho wamesema ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye mafanikio zaidi ya tasnia ya kuku kwa kuwa wamejadili kwa kina namna bora ya kukuza tasnia hiyo ili wananchi wengi zaidi waweze kushiriki katika ufugaji wa kuku ambao unatoa ajira ya moja kwa moja.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya mikutano ya mara kwa mara na wadau mbalimbali wa sekta za mifugo na uvuvi ili kupata maoni yao namna ya kuboresha sekta hizo, ambapo katika kikao hiki cha wadau wa tasnia ya kuku wamekubaliana kufanya kikao kingine Mwezi Septemba mwaka huu ili kufanya tathmini ya namna ya kuboresha zaidi mambo waliyokubaliana yakiwemo ya kuzuia biashara haramu ya mazao ya kuku, ubora na wingi wa vifaranga vya kuku nchini pamoja na uwepo wa nafaka za kutosha kwa ajili ya kutengenezea vyakula vya kuku ili kupunguza gharama za uzalishaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichohusisha baadhi ya wazalishaji wa vifaranga na wafugaji wakubwa wa kuku kilichofanyika jijini Dodoma ambapo amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa sekta binafsi kushiriki katika mnyororo wa ukuzaji uchumi wa taifa ambapo takriban kaya milioni nne zinajihusisha moja kwa moja na ufugaji wa kuku. (22.03.2023)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (katikati), Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Prof. Hezron Nonga (kulia) na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Bw. Stephen Michael (kushoto) wakisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wadau wa tasnia ya kuku wanaozalisha vifaranga na wafugaji wakubwa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma ambapo wameiomba serikali kuangalia ubora na upatikanaji wa vifaranga nchini pamoja na uwepo wa wingi wa nafaka za kuzalisha chakula cha kuku. (22.03.2023)

Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichohusisha wazalishaji wa vifaranga na wafugaji wakubwa kilichofanyika jijini Dodoma, ambapo wamesema wamejadili kwa kina namna bora ya kukuza tasnia hiyo ili wananchi wengi zaidi waweze kushiriki katika ufugaji wa kuku ambao unatoa ajira ya moja kwa moja. Kikao hicho kimeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe. (22.03.2023)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni