Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete na kujadiliana namna wanavyoweza kuendelea kushirikiana katika kuimarisha Sekta ya Mifugo na Uvuvi hapa nchini.
Waziri Ulega alikutana na Mkurugenzi huyo ofisini kwake jijini Dodoma mapema leo Machi 23, 2023.
Katika mazungumzo yao, Waziri Ulega alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa kipaumbele cha Wizara ni kuboresha maisha ya wafugaji na wavuvi na ndio maana kwa sasa wamejikita katika kuanzisha vituo atamizi kwa vijana ili wafanye ufugaji wa kisasa, kuwawezesha vijana kufuga samaki kwa njia ya vizimba katika ukanda wa ziwa Victoria, kukopesha wavuvi maboti ya kisasa ya uvuvi ili waachane na uvuvi wa kuwinda.
Alisema kuwa wavuvi wengi wamekuwa hawapati mavuno ya kutosha, kutokana na vifaa duni vya kufanyia uvuvi, wanavua samaki kati ya kilo 10-100, ni kiasi kidogo ambacho kinaendelea kuwafanya wavuvi wengi kubaki katika umasikini, lakini wakiendelea kupatiwa boti za kisasa uzalishaji katika sekta ya uvuvi utaongezeka na maisha ya wavuvi yatakuwa bora zaidi.
"Hivyo ili wavuvi wetu waweze kufaidika na rasilimali za uvuvi ni muhimu kuwawezesha vifaa vya kisasa ili waweze kuvua katika kina kirefu cha maji wapate mazao ya kutosha kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla", alisema Mhe. Ulega
Kuhusu Sekta ya Mifugo, Waziri Ulega alieleza kuwa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ina maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa malisho na ufugaji na hivyo aliwaomba Benki ya Dunia kuona pia namna ambavyo wanaweza kuwezesha uwekezaji.
Kwenye eneo la udhibiti wa magonjwa, Mhe. Waziri alisema kuwa kwa sasa wanajipanga kuwa na Kampeni kubwa ya Kitaifa ya kuhamasisha uchanjaji wa mifugo ili kupunguza vifo vya mifugo kutokana na magonjwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete alimuhakikishia Waziri Ulega kuwa Benki ya Dunia itaendelea kuimarisha ushirikiano ili kuzifanya sekta hizo mbili ambazo zinategemewa na wananchi wengi kuendesha maisha yao kuzalisha kwa tija na kuondoa umasikini miongoni mwao.
Aliongeza kwa kusema kuwa Benki ya Dunia imekuwa ikifadhili miradi ya Wizara hivyo wako tayari kuendelea kushirikiana ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwainua wananchi wake kiuchumi kupitia sekta hizo mbili.
Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe alisema wako tayari kushirikiana na Benki ya Dunia hususan katika kuongeza ajira za vijana na kina mama kupitia vituo atamizi na ufugaji viumbe maji.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete (wa tatu kutoka kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma Machi 23, 2023. Wa pili kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe. Wengine katika picha ni Wataalam kutoka Wizarani, na Benki ya Dunia.
Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete (wa tatu kutoka kulia) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wanne kutoka kushoto) walipokutana kujadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia. Mhe. Waziri alikutana na Mkurugenzi huyo ofisini kwake jijini Dodoma Machi 23, 2023. Wengine katika picha ni Wataalam kutoka Wizarani na Benki ya Dunia.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiongea na Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete walipokutana kujadiliana namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia katika kuendeleza Sekta ya Mifugo na uvuvi. Mhe. Waziri alikutana na Mkurugenzi huyo ofisini kwake jijini Dodoma Machi 23, 2023.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akieleza jambo kabla ya kumkaribisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) kuongeza na Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete walipokutana kujadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia. Mhe. Waziri alikutana na Mkurugenzi huyo ofisini kwake jijini Dodoma Machi 23, 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni