- Wasema sasa wapo huru kuendelea na shughuli zao za ufugaji na kilimo kwa amani.
WANANCHI wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameipongeza
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 15 na hivyo kuwawezesha
kuendelea kufanya shughuli zao za ufugaji na kilimo kwa uhuru na amani.
Wamesema kumalizika kwa mgogoro huo ambao ulihusisha wakazi
wa wilaya hiyo wanaoendesha shughuli za ufugaji na kilimo katika eneo la Bonde
la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumanne, Januari 17, 2023) baada
ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwatangazia wananchi hao kuwa Serikali imefanya
maboresho makubwa kwenye Tangazo la Serikali namba 28 na kuliacha nje ya mpaka
wa hifadhi eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 74,000 kwa ajili ya kuwawezesha
wananchi hao kufanya shughuli za ufugaji na kilimo. Mkutano huo umefanyika
kijijini Kapunga.
“Tunamshukuru mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia kwa uamuzi
mkubwa alioufanya wa kuboresha GN 28, sasa tutafuga kwa uhuru na kuondokana na
ufugaji wa kuhamahama, pia tunamshukuru kwa uamuzi wa serikali wa kutoa elimu
ya ufugaji wa kisasa na wenye tija watakayopatiwa ambayo inakwenda kuwasaidia
kuongeza mnyororo wa thamani” Amesema Mwenyekiti wa Wafugaji katika ranchi ya
Matebele-Madunguru, Lokordu Siloma.
Kadhalika amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kusikiliza
kero zao na kuzipatia ufumbuzi na sasa wanakwenda kufuga kwa kuzingatia
maelekezo yaliyotolewa. “Awali watu wenye uwezo walikuwa wanavamia maeneo ya
ranchi na kuendesha shughuli za kilimo lakini kwa kauli hii wafugaji tutaachiwa
ranchi zetu tulishe mifugo yetu. Tunaishukuru sana Serikali.”
Naye Elibauti Mwinuka mkulima katika kata ya Itamboleo wilayani
Mbarali amesema kuwa sasa watalima kwa uhuru na kuongeza uzalishaji kwa sababu
awali tulikuwa tunalima kwa wasiwasi.
Anle Kifute ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kapunga
amesema amefurahishwa na kauli ya Serikali ambayo inakwenda kuwaondolea
migogoro katika maeneo yao na hivyo wataweza kuendesha shughuli zao bila ya
usumbufu wa aina yoyote.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Majaliwa baada ya kutangaza
maamuzi hayo ya Serikali, amewataka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Zuberi Homera na
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune wahakikishe wanasimamia vizuri sheria
pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa
vyanzo vya maji.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mashimba Ndaki pamoja na viongozi wa Ranchi za Taifa waende kwenye Ranchi ya
Usangu na kuwapanga upya wafugaji ili manufaa ya ufugaji yaonekane ikiwemo
uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.
Amesema Serikali imefanya maboresho hayo kwa lengo la
kuwawezesha wafugaji na wakulima wilayani humo kuendesha shughuli kitaalamu na
kuwaongezea tija. “Marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha baadhi ya vitongoji
vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka na
kutumiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo.”
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amemuhakikishia
Waziri Mkuu kuwa Wizara itakwenda kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa juu ya
matumizi ya Ranchi ya Usangu ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wale wote wanaoitumia
ranchi hiyo kinyume na makubaliano yaliyowekwa.
Aidha, amesema kuwa Wizara itashirikiana na wafugaji
kuhakikisha miundombinu ya ufugaji unajengwa na kuboreshwa katika eneo hilo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera, wakati alipofanya ukaguzi wa hali ya hifadhi ya usangu, Ranchi ya Usangu, Ihefu, Madibila, Ubaruku na Kapunga, Januari 17, 2023. Ukaguzi huo unafuatia maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya marekebisho kwenye tangazo la Serikali namba 28 ambalo limetoa hekta 74,000 kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu. Kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula. (17.01.2023)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia waliosimama) akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Kapunga wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ambapo amewataka wafugaji kutumia Ranchi ya Usangu kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kuanza kufuga kisasa. (17.01.2023)
Baadhi ya viongozi na wadau walioshiriki kikao cha wadau kilichotoa maamuzi juu ya matumizi endelevu ya bonde la usangu, ambapo aliwasihi wadau hao kufuata na kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa.
Baadhi ya viongozi na wadau walioshiriki kikao cha wadau kilichotoa maamuzi juu ya matumizi endelevu ya bonde la usangu, ambapo aliwasihi wadau hao kufuata na kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa.
Wananchi wa eneo
Kapunga, Wilaya ya Mbalali Mkoani Mbeya, walimsikiliza Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akizungumza kuhusu maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya
marekebisho kwenye tangazo la Serikali namba 28 ambalo limetoa hekta 74,000 kwa
wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu. (17.01.2023)
Muonekano wa baadhi ya maeneo ambayo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu. Rais Dkt. Samia ameridhia kufanya marekebisho kwenye tangazo la Serikali namba 28 ambalo limetoa hekta 74,000 kwa ajili ya wananchi. (17.01.2023)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni