Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema ni wakati sasa kwa wafugaji kupimiwa ardhi na kupatiwa hati ili waweze kumiliki maeneo yao kisheria na kufuga kisasa ili kukuza Sekta ya Mifugo nchini.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (24.10.2022) katika Kitongoji cha Nkanka, Kijiji cha Itumba Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, wakati akizungumza na wanakijiji kufuatia Kamati ya Mawaziri wanane wa Kisekta kufika katika kijiji hicho ikiwa ni moja ya vijiji 975 kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Akichangia ripoti ya kamati hiyo Naibu Waziri Ulega ameeleza kuwa kwa sasa soko la nyama limekuwa kubwa nje ya nchi, hivyo ni vyema Mkoa wa Songwe ukajipanga vyema ili kutumia fursa hiyo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amelifungua.
"Baada ya utatuzi wa migogoro ya ardhi baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ni lazima kutengwa maeneo ya mifugo na kuwamilikisha ardhi wafugaji kwa kuwapatia hati kwani kwa kufanya hivyo, itasaidia katika kuyalinda maeneo hayo kwa ajili ya uzalishaji na ufugaji wa kisasa wenye kuleta tija na kukidhi mahitaji makubwa ya soko la nyama ndani na nje ya nchi." Amesema Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa kila eneo la mifugo linapaswa kuandikishwa kwenye gazeti la serikali kwa mujibu wa sheria ili lisigeuzwe matumizi, pia maeneo ya wafugaji wanapomilikishwa yatawawezesha kupata mikopo katika mabenki ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB).
Aidha, amesema hatua hiyo itaiwezesha serikali kuyasajili na kuyatangaza kama ni maeneo ya ranchi hivyo kurahisisha biashara ya mifugo na nyama ndani na nje ya nchi.
Awali, akichangia hoja mbalimbali wakati wa kikao kilichofanyika katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, kilichohusisha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Mhe. Dkt. Angeline Mabula, Naibu Waziri Ulega amesema ni wakati sasa kwa wafugaji kuthaminiwa na kupatiwa maeneo na kumilikishwa kisheria ili wafuge kisasa.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari imeandaa Mwongozo wa Malisho wa Mwaka 2021 ambao umezinduliwa katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Mwezi Desemba Mwaka 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumzia umuhimu wa utolewaji wa Hati za Ardhi kwa maeneo ya mifugo ili kukuza soko la nyama ndani na nje ya nchi (Oman, Saudia Arabia n.k) ambapo wafugaji wataweza kufuga kisasa. Naibu Waziri Ulega amezungumza hayo kwenye kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe kuhusu utatuzi wa Migogoro ya Ardhi nchini. (24.10.2022)
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb) akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe kuhusu utatuzi wa Migogoro ya Ardhi nchini. Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani). (24.10.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb), akichangia jambo wakati wa kikao cha Mawaziri wa Kisekta na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe kuhusu utatuzi wa Migogoro ya Ardhi katika Vijiji 975 nchini. (24.10.2022)
Picha ya baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao cha Mawaziri wa Kisekta na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe ambapo kikao hicho kimejadili maeneo manane (8) ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kufanyiwa kazi ili kutatua migogoro ya ardhi nchini. Kikao hicho kimefanyika katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb). (24.10.2022)
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb), (wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya mawaziri wa kamati hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wa tatu kutoka kulia) mara baada ya kufika katika Kitongoji cha Nkanka, Kijiji cha Itumba kilichopo Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwemo ni sehemu ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. (24.10.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akizungumza na baadhi ya wanakiji cha Itumba kilichopo Kitongoji cha Nkanka katika Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, baada ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta kufika kijijini hapo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, ambapo amesema serikali imekubali kuwapatia sehemu ya eneo la hifadhi katika kijiji hicho na kuweka makazi ya kudumu huku akitaka wafugaji wapimiwe eneo maalum la shughuli zao na kupatiwa hati ili wamiliki kisheria na kufuga kisasa. (24.10.2022)
Baadhi ya wanakijiji cha Itumba Kitongoji cha Nkanka katika Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, waliohudhuria kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta iliyofika kijijini hapo ikiwa ni moja ya vijiji ambavyo kamati inavitembelea ili kutatua migogoro ya ardhi baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. (24.10.2022)
Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb.) Waziri wa Ardhi na Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kisekta akiongoza Kamati hiyo kuelekea Uwandani kukagua maeneo ya bonde la Usangu lililopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya. Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo ya Mawaziri wa Kisekta (25.10.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni