Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa upande wa Sekta ya Mifugo imeendesha warsha ya siku moja kwa ajili ya kuwawezesha Waelimisha rika wake elimu inayohusu Mwongozo wa kudhibiti virusi vya Ukimwi, Ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukizwa mahala pa kazi tukio lililofanyika leo (10.11.2022) Makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa sekta hiyo Dkt. Charles Mhina ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa mafunzo hayo ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ili kuimarisha afya za watumishi wake wanapokuwa kazini.
“Kama Wizara tuliona umuhimu wa kuwa na mafunzo haya kwa sababu mtapewa elimu ya namna ya kujikinga au kujizuia na haya magonjwa yasiyoambukizwa ambayo kwa sehemu kubwa huwa yanatokana na mitindo ya maisha yetu wenyewe hivyo sasa mtapata fursa ya kujifunza na kuelewa mambo yote na maelekezo yaliyopo kwenye muongozo ule yanayopaswa kutekelezwa” Ameongeza Dkt. Mhina.
Akiwasilisha kuhusu mada inayohusu wazo la Serikali la kuanzisha Mwongozo huo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Bi. Neema Range amesema kuwa afya ya mtumishi wa umma ni kipaumbele kwa Serikali na wananchi anaowahudumia na pale anapokumbwa na maradhi mbalimbali hasara huanzia kwake na Taifa kwa ujumla huku wananchi wakikumbana na changamoto ya kukosa huduma.
“ Afisa mmoja tu anapokuwa na ratiba ya kuhudhuria kliniki hata mara 3 tu kwa wiki kutokana na maradhi mbalimbali yanayomkabili, husababisha idadi kubwa ya wananchi kukosa huduma huku yeye pia akiyumba kiuchumi kutokana na kutumia gharama kubwa kwenye matibabu hayo na ndio maana Serikali iliona upo umuhimu wa kuanzisha mwongozo huu ili kupunguza hatari ya kukumbwa na Virusi vya Ukimwi, Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa kwa watumishi.
Naye Daktari kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa jiji la Dodoma Dkt. Revocatus Baltazary amebainisha kuwa hadi sasa zaidi ya asilimia 60 ya watanzania wakiwemo watumishi wa Umma wanaathiriwa na magonjwa yasiyoambukizwa ambapo ametoa rai kwa wananchi hao kubadili mitindo yao ya maisha jambo alilobainisha kama chanzo kikuu cha tatizo hilo.
“Unakuta mfanyakazi anashinda amekaa kwenye kiti chake kwa muda mrefu sana na akitoka hapo anaingia kwenye gari lake hadi nyumbani au sehemu flani kukutana na ndugu jamaa na marafiki na kabla hajalala anakula chakula cha wanga kwa wingi sasa ndipo anaenda kulala bila hata kufanya mazoezi, hapo ni lazima akumbane na magonjwa haya yasiyoambukizwa ambayo yamekuwa hatari zaidi kuliko yale ya kuambukizwa” Amefafanua Dkt. Baltazary.
Mwongozo wa kudhibiti virusi vya Ukimwi, Ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukizwa mahala pa kazi uliasisiwa mwaka 2007 ambapo ulikuwa ukijulikana kama Mwongozo wa kudhibiti virusi vya ukimwi na Ukimwi huku ukiwa na lengo la kupunguza kasi ya maambukizi ya Virusi vya ukimwi kwa watumishi wa umma kabla ya kuboreshwa na kuongezwa magonjwa sugu yasiyoambukizwa.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo na waelimisha rika kutoka idara na vitengo vya sekta ya Mifugo muda mfupi baada ya Dkt. Mhina kufungua mafunzo ya Mwongozo wa kudhibiti virusi vya Ukimwi, Ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukizwa mahala pa kazi kwa waelimisha rika hao yaliyofanyika leo (10.11.2022) Makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Neema Range akiufafanua Mwongozo wa kudhibiti virusi vya Ukimwi, Ukimwi na Magonjwa yasiyoambukizwa mahala pa kazi wakati wa mafunzo kwa waelimisha rika kutoka Sekta ya Mifugo yaliyofanyika leo (10.11.2022) kwenye Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Daktari kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa jiji la Dodoma Dkt. Revocatus Baltazary akitoa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa wakati wa mafunzo kwa waelimisha rika kutoka Sekta ya Mifugo yaliyofanyika leo (10.11.2022) kwenye Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni