Na Mbaraka Kambona,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kujenga Majosho ya kuogeshea Ng'ombe 178 ili kuiepusha mifugo na magonjwa yanayosababishwa na Kupe na maradhi mengine yanayoambatana na kutokuogesha mifugo hiyo.
Waziri Ndaki aliyasema hayo katika ziara yake ya kukagua miundombinu ya majosho iliyopo katika Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara Disemba 11, 2021.
Akiongea na Wafugaji wanaofanya shughuli zao katika Vijiji vya Salamakati na Kisarakwa vilivyopo katika Wilaya hiyo alisema kuwa lengo la Serikali ni kuweka josho kwenye kila Kijiji kilicho na Ng'ombe.
"Josho ni Zahanati ya Mifugo, hivyo sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunataka tuweke kila mahali ili wafugaji waweze kuogesha mifugo yao kuepukana na Kupe na magonjwa mengine yanayotokana na kutokuogesha mifugo," alisema
Aliongeza kuwa mipango iliyopo ni kuendelea kuifanya mifugo iwe na afya njema jambo ambalo litasaidia kuongeza tija katika ufugaji ikiwemo kuuza mifugo hiyo kwa bei nzuri.
Aidha, Waziri Ndaki aliwataka wafugaji hao na Wananchi kwa ujumla kuendelea kutunza miundo mbinu ya majosho iliyopo katika maeneo yao na ile itakayojengwa kwa sababu kwa kufanya hivyo kutasaidia uogeshaji wa mifugo kuwa endelevu.
Naye, Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere alimuomba Waziri Ndaki kuhamishia hela za ujenzi wa majosho katika Halmashauri ili iwe rahisi kuzifuatilia tofauti na ilivyo sasa ambapo hela za ujenzi zinatoka Wizarani jambo ambalo linaleta ugumu katika ufuatiliaji wake na hivyo kupelekea miradi ya ujenzi wa majosho kuchelewa kumalizika.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (aliyeshika fimbo)
akiswaga Ng'ombe kuelekea kwenye josho kwa ajili ya kuwaogesha katika Josho la
Mekomariro lililopo Wilayani Bunda, Mkoani Mara Disemba 11, 2021. Waziri Ndaki
alikuwa Wilayani humo kukagua miundombinu ya Majosho ambapo aliwataka wafugaji
kutunza miundombinu ya majosho ili kufanya uogeshaji wa Mifugo kuwa endelevu.
Kulia kwake (mwenye shati Jeupe) ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua
Nassari.
Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Wafugaji wa Kijiji cha Sarakwa muda
mfupi baada ya kuzindua Josho la kuogeshea Mifugo lililojengwa katika
Kijiji hicho Disemba 11, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni