Nav bar

Jumatatu, 10 Januari 2022

WANAWAKE MKURANGA WAISHUKURU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KUWAPATIA MRADI WA KUKU

Jukwaa la wanawake Mkuranga Mkoa wa Pwani wameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwawezesha vikundi vya wanawake Wilayani Mkuranga ufadhili wa kuku  kwa ajili ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi

Akitoa shukrani za wanawake hao Disemba 11,2021 Wilayani  Mkuranga,  mwenyekiti wa jukwaa hilo, Bi. Mariam Ulega amesema kuwa hatua ya Wizara hiyo kuwawezesha wanawake kunaendana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kuliletea taifa maendeleo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

Alisema kwa sasa wanawake wengi wameamua kuondokana na suala la utegemezi kwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali hasa za ujasiriamali hivyo nafasi ya mwanamke katika kuchangia kukuza uchumi wa nchi ni mkubwa.

"Tumepokea kuku lakini tuhakikishe kuku tunawalea na tunawatunza kama tunavyowatunza watoto wetu kwa sababu hiki ni chanzo cha uchumi na mwanamke bila uchumi huwezi kusonga mbele ni lazima ujikomboe kiuchumi ili uwakomboe na wenzako, kwa hiyo tunashukuru sana wizara kwa kutuwezesha" alisema 

Mkurugenzi Msaidizi Mafunzo na Ugani, Dkt. Hassan Mruttu alibainisha kuwa utoaji wa vifaranga hivyo ni mradi wa shamba darasa kwa wafugaji wa kuku ambapo unatarajiwa kutekelezwa nchi nzima

Alisema kwa sasa wameamua kuanza na vikundi viwili ambavyo awali walianza kuvipatia mafunzo ambapo wataendelea na shamba darasa kwa kuwashirikisha katika hatua zote za ufugaji bora na watapatiwa cheti.

"Haya mashamba darasa ya kuku tunatazamia kufanya nchi nzima lakini kwa kuanzia Mkuranga ni kwa sababu tulitoa mafunzo kabla na kuwaletea vifaranga lakini baadae tukagundua kwamba haikuwa mashamba darasa bali mashamba ya mfano kwamba wanakuja kuangalia tu badala ya kushirikishwa kwenye ufugaji bora kama tunavyofanya sasa" alisema

Aliongeza kuwa utaratibu wa sasa utakuwa unaanza ngazi ya awali mpaka kufikia kuzalisha vifaranga wengine na kufanya kuwa ufugaji endelevu ambapo pia vyeti watakavyopata vitawasaidia katika kutafuta huduma za kifedha ikiwemo mikopo.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Mhe. Subira Mgalu aliwataka wanawake hao kutumia kuku hao vizuri ili kujikwamua kiuchumi.

Alisema Serikali imetumia gharama kubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi hivyo kama kuku hao watatumika tofauti na malengo tarajiwa watakuwa wamerudisha nyuma jitihada za Serikali ya Rais Mhe. Samia Hassan katika kumkomboa mwanamke.


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Mhe. Subira Mgalu akipokea kuku kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Mkuranga, Bi. Anna Kiria (kulia) kwa ajili ya kuzigawa kwenye vikundi vya wanawake wa Mkuranga. Lengo likiwa ni kuwasaidia kuweza kujikwamua kiuchumi. 

Sehemu ya washiriki wa jukwaa la wanawake wa Wilaya ya Mkuranga walioshiriki katika zoezi la ugawaji wa kuku Mkoani Pwani. Disemba 11, 2021. 

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni