Nav bar

Jumatatu, 10 Januari 2022

SERIKALI YAANZA KUFANYA TATHMINI YA SERA YA TAIFA YA MIFUGO

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Mifugo imeanza kufanya tathmini za utekelezaji wa Sera ya Taifa ya  Mifugo ya mwaka 2006 kwa lengo la kubaini changamoto na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia na kiuchumi  yaliyojitokeza wakati wote wa  utekelezaji wa sera hiyo.

Tathmini hiyo imeanza kufanyika leo (13.12.2021) Mkoani Arusha  kwa upande wa  kanda ya Kaskazini ambapo zaidi ya wadau 62 kutoka katika Mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wamehudhuria na kutoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa sera hiyo.

Akizungumzia kwa kifupi lengo la kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza amesema kuwa Wizara inaamini kwa kipindi cha miaka 15 tangu kuanza kutekelezwa kwa sera hiyo kuna changamoto kadhaa za kisera ambazo wataalam wamekuwa wakikumbana nazo hivyo Wizara itazikusanya zote na kuangalia namna ya kufanya marekebisho ya Sera hiyo.

“Tathmini hii tumeanzia kanda ya kaskazini lakini kuanzia mwezi Januari tutaelekea na kwenye kanda nyingine na tutashirikisha wadau wote muhimu waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yanayotokana na mifugo na lengo letu ni kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za ufugaji haukwamishwi na changamoto zozote za kisera” Ameongeza Dkt. Asimwe.

Wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Mgeni rasmi ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Athuman Kihamia alibainisha mafanikio yaliyopatikana kupitia Sera ya Taifa ya Mifugo iliyopo hivi sasa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya Mifugo kwenye pato la taifa, kuongezeka kwa idadi ya mifugo, kuongezeka kwa idadi ya viwanda vya maziwa kutoka 22 mwaka 2006 hadi 105 mwaka 2021, kuongezeka kwa uwekezaji katika machinjio za kisasa na  kuongezeka kwa Viwanda vya nyama kutoka kiwanda kimoja mwaka 2006 hadi 11 mwaka 2021.

“Lakini pia kama tunavyofahamu kwenye mafanikio hapakosi changamoto hivyo moja ya changamoto zilizoikumba sekta ya mifugo wakati wote wa utelelezaji wa sera hiyo ni wafugaji kushindwa kutekeleza teknolojia zinazoendana na wakati, nyingine ni uwepo wa mbari za mifugo ambazo hazileti tija inayohitajika, uwepo wa watoa huduma wa pembejeo za mifugo wasiokidhi vigezo na uwepo wa magonjwa mbalimbali yanayoathiri mifugo” Amesema Dkt. Kihamia.

Awali, Mtaalam wa mnyororo wa thamani kwa upande wa Mifugo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO) Dkt. Moses Ole-Noselle amesema kuwa Shirika hilo lipo tayari kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika mchakato huo wa tathmini ya Sera ya Taifa ya Mifugo ambapo amebainisha kuwa lengo la Shirika hilo ni kuhakikisha wafugaji wanafanya shughuli zao kwa tija na hali zao za kiuchumi zinaendana na idadi ya mifugo iliyopo hapa nchini.

Mbali na Viongozi na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kikao hicho kimejumuisha pia wataalam wa Mifugo kutoka Mamlaka za Serikali  za mitaa zilizopo kanda ya kaskazini, wazalishaji na wachakataji wa mazao yanayotokana na mifugo na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza akielezea lengo la Wizara kufanya tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mifugo wakati wa kikao cha kanda ya kaskazini cha tathmini ya Sera hiyo kilichofanyika (13.12.2021) jijini Arusha.

Mtaalam wa Mnyororo wa thamani kwa upande wa Mifugo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO), Dkt. Moses Ole-Neselle akiihakikishia Serikali ushirikiano kutoka kwenye shirika lake wakati wa kikao cha kanda ya kaskazini cha tathmini ya  utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mifugo kilichofanyika  (13.12.2021) jijini Arusha. 

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni