Nav bar

Alhamisi, 1 Julai 2021

MDAHALO WA KUKUSANYA MAONI YA WADAU JUU YA MIFUMO YA USALAMA WA CHAKULA NCHINI WAZINDULIWA KANDA YA ZIWA.

 

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi) Bw. Amos Machilika amezindua mdahalo wa mifumo ya usalama wa  vyakula katika kanda ya ziwa, lengo likiwa ni kukusanya maoni ya wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi ili kuboresha mifumo hiyo inayoendana na ajenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Julai  1,  2021,  Bw. Machilika  alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimetia saini makubaliano ya kutekeleza malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).

Alisema Serikali inatambua mfumo wa Usalama wa chakula una changamoto zilizoenea duniani zikiwamo mabadiliko ya hali ya hewa, magonjwa sugu, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ukosefu wa usawa wa kijamii, hivyo mjadala huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto hizo.

“Nimeambiwa kwamba mijadala hii itaongozwa na maswali yaliyoandaliwa kulingana na maeneo ya vipaumbele ambapo kwa kila changamoto mapendekezo ya hatua za kuboresha zitaainishwa, hii itasidia sana kufikia malengo ya SDGs,” alisema Bw. Machilika.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kuwa na mijadala ya mifumo ya chakula na kuanzisha mchakato wa ushirikishaji wadau wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Alisema lengo ni kubainisha namna ambavyo mifumo ya chakula inaweza kuboreshwa ili kuleta maendeleo ya haraka.

“Mijadala mbalimbali itaendeshwa nchini, majumuisho yatafanyika ili kuwa na mapendekezo ya nchi na hatua za kuimarisha mifumo ya Usalama wa chakula ambayo ni endelevu.

Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa katika Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Mjini New York- Marekani, mwezi Septemba, 2021.”


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Amos Machilika akifungua mdaalo  wa kujadili mifumo ya usalama  wa  vyakula Nchini kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa Julai 1, 2021 Mkoani Mwanza.

Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa vyakula kutoka Wizara ya Kilimo ambae pia ni Mratibu wa Kitaifa wa kongamano la kuboresha  mifumo ya Chakula Duniani inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa (UNFSS), Dkt. Honest Kessy akiwasilisha mada ya namna ya kuendesha midaalo hiyo, iliyofanyika  Julai 1, 2021 kwenye ukumbi wa Gold Crest Mkoani Mwanza.

 

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Amos Machilika (wa pili kutoka kulia mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa  kongamano  la kujadili mifumo ya usalama  wa  vyakula Nchini kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa  lililofanyika  Julai 1, 2021 Mkoani Mwanza.

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni