Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzalisha kwa wingi vifaranga wa samaki ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na fursa ya ufugaji wa samaki ambayo imeonekana kuvutia watu wengi kwa hivi sasa.
Mhe. Samia ameyasema hayo wakati
akiwaapisha Makatibu wakuu wa Wizara na watendaji wa taasisi mbalimbali
aliowateua hivi karibuni tukio lililofanyika leo (06.04.2021) Ikulu ya Mkoa wa Dar-es-salaam ambapo
ameitaja njia hiyo ya ufugaji wa samaki kama “bluu economy” ya watu wa chini.
“Lakini pia tumeharibu sana mazingira
ya bahari kiasi kwamba kupata samaki ni mpaka mvuvi afike maeneo ya bahari kuu
hivyo tunaweza kuyatumia maeneo ya pembeni kuweka vizimba ili watu wengine
waendelee na uchumi wao wa blue” Amesisitiza Mhe. Samia.
Kwa upande wa sekta ya Mifugo, Mhe.
Samia amesema kuwa Wizara ina wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa mbegu bora za Mifugo pamoja na
kusimamia masoko ya wafugaji huku pia akiitaka
kusimamia ubora pindi wafugaji wanapochinja mifugo yao.
“Ukienda Arabuni wanataka sana nyama kutoka Tanzania lakini kiwango
wanachokitaka sio kiwango tunachozalisha kwa sababu uzalishaji wetu upo chini
sana na “quality” yetu ipo chini sana” Ameongeza Mhe. Samia.
Mhe. Samia ameiagiza Wizara hiyo
kuendelea kutoa mafunzo kwa wafugaji kuhusu njia bora na za kisasa za ufugaji
ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya unenepeshaji wa mifugo kutoka hatua ya awali
mpaka anapelekwa machinjioni na kuwataka wafugaji kote nchini kuachana na
ufugaji wa zamani usio na tija.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia
sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah ni miongoni mwa Watendaji walioteuliwa
hivi karibuni na kuapishwa leo kwenye hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni