Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki leo amewaongoza viongozi, watendaji na watumishi wa Wizara hiyo kumpokea Naibu Waziri wake Mhe. Abdallah Ulega tukio jioni ya leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Mara baada ya kumpokea Mhe. Ulega, Mhe.
Mashimba alitumia fursa hiyo kumueleza malengo mbalimbali ambayo Wizara hiyo ilipangiwa kuyatekeleza ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanaondokana na umasikini na sekta
hizo zitengeneze ajira za kutosha hasa ikizingatiwa kuwa ni sekta za
uzalishaji.
“Karibu sana, bahati nzuri wewe ni
mwenyeji hivyo nina uhakika tutaongeza tija katika kuhakikisha tunawavusha
salama wafugaji na wavuvi na tunaongeza mchango wa kutosha kwenye pato la taifa
kwa sababu mpaka sasa sekta hizi mbili mchango wake ni mdogo sana” Alisisitiza
Mhe. Ndaki.
Huku akionekana mwenye furaha Mhe.
Ulega aliwashukuru watendaji mbalimbali wa Wizara hiyo kwa salamu nyingi za
pongezi walizomtumia tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo ambapo aliwaahidi
kuwapa ushirikiano wa kutosha katika utendaji wao wa kila siku.
“Nimerudi nyumbani na kwa kweli
nimefurahi sana, nataka niwahakikishie tu nimekuja hapa ili tushirikiane kwa
pamoja kwa ajili ya kutekeleza malengo ambayo Mhe. Rais anayatarajia kupitia
sekta za Mifugo na Uvuvi” Aliongeza Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega ameahidi kumpa ushirikiano
wa kutosha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki huku pia akiwa na
matumaini kuwa ushirikiano wao utaleta tija kwenye sekta zote mbili za Mifugo
na Uvuvi.
Akitoa maelezo ya Utangulizi, Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel mbali na
kumkaribisha Mhe. Ulega kwa mara nyingine tena wizarani hapo aliahidi kumpa
ushirikiano wa kutosha wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo na
kumhakikishia kuwa watumishi wote wa sekta ya Mifugo wapo tayari kufanya hivyo
pia.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Mhe. Ulega pamoja na
kuwa ni kiongozi, kwenye sekta ya uvuvi amekuwa mtaalam mwenzao na mara zote
walishirikiana naye katika shughuli mbalimbali za sekta hiyo hivyo kurejea
kwake kwao imekuwa ni kama bahati.
“Kwa kweli hata niliposikia unarejea
tena kwa sababu hata wakati ule tulikuwa hatukutumii tu kama Waziri bali
mtaalam wa sekta ya Uvuvi kwa hiyo tuna uhakika kurejea kwake kutasaidia
shughuli za uvuvi kuendelea zaidi” Alihitimisha Dkt. Tamatamah.
Mhe. Ulega anarejea Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kama Naibu Waziri wa Wizara hiyo kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya
kumuapisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango
jana (31.03.2021).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia) na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Makatibu wakuu wa Wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel anayeshughulikia sekta ya Mifugo (kushoto) na Dkt. Rashid Tamatamah anayeshughulikia sekta ya Uvuvi (kulia) wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Mhe. Ulega Wizarani hapo tukio lililofanyika leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akifafanua malengo ambayo Wizara yake imepangiwa kuyatekeleza mbele ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega muda mfupi baada ya kumkaribisha wizarani hapo tukio lililofanyika leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega wakiwa wameshikana mikono kama ishara ya Mhe. Ndaki kumkaribisha Mhe. Ulega Wizarani hapo tukio lililofanyika leo (01.04.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kukaribishwa na kuingia ofisini kwake leo makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma leo (01.04.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni