Wachunaji wa ngozi katika machinjio ya Manispaa ya Tabora wametakiwa kutumia mbinu bora na vifaa stahiki wakati wa uchunaji wa ngozi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi
wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura
leo (08.04.2021) wakati akifungua mafunzo kwa wachunaji hao yaliyofanyika
katika eneo la Machinjio hiyo.
Bura amesema kumekuwa na uharibifu mkubwa
wa ngozi unaotokana na kukosekana kwa matumizi ya mbinu bora, vifaa stahiki na umakini
katika uchunaji ambapo ngozi kuchunwa vibaya na nyingine na hivyo kupoteza
ubora unaotakiwa katika viwanda.
"Ngozi ni moja kati ya mazao ya
mifugo yanayoliingizia taifa fedha nyingi lakini kutokana na uchunaji mbovu mnasababisha
ngozi nyingi kutofaa kwa matumizi ya viwanda wakati mahitaji ya viwanda ni
makubwa," alisema Bura.
Aidha, Bura aliwaeleza kuwa baada ya
mafunzo hayo ya kupeana mbinu bora za uchunaji na matumizi ya vifaa stahiki, watatakiwa
kujaza fomu kwa ajili ya kupatiwa leseni na endapo mchunaji hatakuwa na leseni
hataruhusiwa kuingia machinjioni kufanya shughuli za uchunaji. Na ni matarajio
ya wizara na wenye viwanda kuwa kuanzia sasa watakuwa wakichuna ngozi kwa
kufuata maelekezo waliyopatiwa.
Vilevile amesema katika kuikagua
machinjio hiyo amebaini ubovu wa sakafu ambao kama usiporekebishwa nao ni
chanzo cha uharibifu wa ngozi hasa pale ng'ombe anapovutwa baada ya kuchinjwa.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa
manispaa ya Tabora ambaye pia ni Afisa Mifugo, Neema Kapesa amesema mafunzo
hayo ni muhimu sana kwao kama wataalam wa halmashauri na kwa wachunaji.
Bi. Kapesa amesema sasa watahakikisha
taratibu zinazotakiwa zinafuatwa na wachunaji katika kuchuna ngozi na endapo
mchunaji ataharibi ngozi watamchukulia hatua. Lakini pia ameahidi kumfikishia
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo tatizo la miundombinu hasa kwenye sakafu ili aone
namna ya kulitatua kwani haitakuwa vizuri Manispaa ikawa ndio chanzo cha
uharibifu wa ngozi kutokana na ubovu wa sakafu.
Afisa Masoko na Mahusiano kutoka
Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro, Fredrick Njoka amesema wameamua kushirikiana
na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) kutoa elimu kuhusu mbinu bora za
uchunaji ngozi na matumizi ya vifaa stahiki kwa kuanza na wachunaji kwa kuwa
imebainika asilimia kubwa ya ngozi huaribika machinjioni.
Njoka amesema mahitaji ya ngozi katika viwanda ni makubwa na ili wazalishe bidhaa bora ni lazima wapate ngozi bora. Hivyo elimu hii wataendelea kushirikiana na wizara kuitoa katika mikoa mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni