Na. Edward Kondela
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe.
Jeroen Verheu amesema nchi yake iko tayari kusaidia ujenzi wa vituo vya mafunzo
ya ufugaji samaki nchini ili kuunga mkono mkakati wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
kuhakikisha inafikisha huduma za mafunzo hayo kila wilaya.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki akizungumza jana (10.04.2021), mara baada ya kufanya mazungumzo na balozi
huyo katika ofisi ndogo za wizara zilizopo jijini Dar es Salaam, amesema Mhe.
Balozi Verheu ameridhishwa na mkakati wa wizara ambapo katika bajeti ya mwaka
wa fedha 2021/22 imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo arobaini vya
mafunzo ya ufugaji samaki.
“Sisi kama wizara tumeanza na mkakati
huo na tumetenga fedha kwa ajili ya vituo arobaini katika bajeti ijayo na
kwamba wamesema wako tayari kusaidia kwa kuweka vituo vingine zaidi, tunataka
kuweka vituo vya mafunzo kila wilaya kwa ajili ya wafugaji wa samaki wapate
mahali pa kujifunza badala ya kwenda kwenye vituo ambavyo viko mbali.” Amesema
Mhe. Ndaki
Kuhusu uchumi wa bluu Waziri Ndaki
amesema balozi huyo amemhakikishia wanaweza kuisaidia Tanzania kupitia mpango
wao maalum ujulikanao “Global Development Program” ambao unalenga kusaidia nchi
zinazoendelea kwenye masuala ya uchumi wa bluu na kuiomba wizara iangalie
maeneo ambayo inaweza kunufaika kupitia mpango huo.
Aidha, Mhe. Balozi Verheu ameisifia
Zanzibar kwa hatua ilizofikia kuhusu uchumi wa bluu, huku Waziri Ndaki
akimhakikishia pia Tanzania Bara imeweka malengo ya kutengeneza uchumi
unaotokana na Bahari ya Hindi, maziwa na mabwawa.
Pia, katika Sekta ya Mifugo Balozi wa
Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu ameonesha nia yake kubwa namna nchi
yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi wa pande zote mbili.
Waziri Ndaki amefafanua kuwa Uholanzi
iko tayari kusaidia maeneo ya malisho ya mifugo pamoja na ushirikiano wa
kitaalamu kwa kutoa utaalamu kwa watanzania nao kupata utaalamu kutoka kwa
watanzania juu ya sekta ya mifugo.
“Nchi ya Uholanzi wameendelea sana
katika tasnia ya maziwa na wamesema wako tayari kushirikiana na Tanzania katika
kukuza soko la maziwa na wazalishaji wa maziwa ambapo hawako rasmi takriban
asilimia 98, tunaweza kuwafanya hao wazalishaji wakawa rasmi na maziwa yao
yakasaidia nchi kimaendeleo.” Amefafanua Mhe. Ndaki.
Katika mazungumzo hayo Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen
Verheu wamekubaliana kuongeza wigo zaidi wa ushirikiano katika sekta za mifugo
na uvuvi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akisalimiana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu, mara baada ya balozi huyo kufika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es salaam, kwa ajili ya mazungumzo na Waziri Ndaki ambapo wamekubaliana kuongeza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta za mifugo na uvuvi. (10.04.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akimsindikiza Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu mara baada ya kuwa na mazungumzo naye katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es salaam, ambapo katika sekta ya mifugo wamekubaliana kuhakikisha asilimia 98 ya wazalishaji maziwa nchini wasio rasmi wanakuwa rasmi katika kukuza maendeleo ya nchi. (10.04.2021)Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es salaam, ambapo balozi huyo amemhakikishia Waziri Ndaki nchi yake inaunga mkono mkakati wa wizara kujenga vituo vya mafunzo ya ufugaji samaki kila wilaya. (10.04.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni