Nav bar

Alhamisi, 4 Februari 2021

WAZIRI NDAKI: "Kuanzia leo wakamateni watuhumiwa 67 wanaotorosha mifugo."

Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameliagiza jeshi la polisi nchini kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo, kuwasaka na kuwamakata mara moja watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake.

 

Waziri Ndaki amebainisha hayo leo (26.01.2021) mjini Dodoma, katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo katika mji wa serikali Mtumba wakati akiwasilishiwa ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani ambapo ripoti hiyo imebaini utoroshaji wa mifugo na mazao yake kwenda nchi za jirani.

 

Amefafanua kuwa serikali haiwezi kuvumilia uwepo wa watu wenye nia ovu kwa kutorosha rasilimali za nchi pamoja na kutoa onyo kwa watu wengine ambao wanatorosha mazao ya mifugo na mazao yake pamoja na wale wenye nia ya kufanya hivyo.

 

“Watoroshaji wa mifugo na mazao yake waanze kukamatwa kuanzia leo, wakamatwe mara moja tuanze na hawa 67 ambao wanajulikana walipo.” Amesema Waziri Ndaki wakati akimuagiza Kamishna Msaidizi wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini Yusuph Sarungi.

 

Aidha, amewaonya wafanyabiashara ambao wanajihusisha na utoroshaji wa mifugo na mazao yake waanze kutafuta kazi nyingine ya kufanya kwa kuwa wizara haitavumilia mtu yeyote ambaye atajihusisha na vitendo hivyo kwa kuwa vinaenda kinyume na sheria za nchi na kuikosesha serikali mapato.

 

Pia, kuhusu urasimu na utoaji wa vibali mbalimbali vya mifugo na mazao yake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewataka watumishi wa wizara waliopo kwenye minada ya upili na mipakani kuacha urasimu wa kuchelewesha kutoa vibali mbalimbali na kuagiza kupatiwa orordha ya watumishi hao na viongozi wao na muda waliohudumu katika ofisi hizo na kuwachukulia hatua za kinidhamu watakaobainika kwenda kinyume na utaratibu wa kazi.

 

"Nataka nipatiwe taarifa za watu hao kuanzia vyeo vyao, umri wao na muda waliohudumu kwenye minada husika ili tuweze kuboresha kwenye eneo kwa sababu utaratibu wa kufanya kazi kwa mazoea umeshapitwa na wakati." Amefafanua Mhe. Ndaki

 

Ili kuhakikisha mifugo na mazao ya mifugo hayatoroshwi kuelekea nchi za jirani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemuagiza Katibu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kuchambua ripoti hiyo na kuainisha mapendekezo yaliyotolewa ili sekta ya mifugo iweze kuwa na mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa.

 

Waziri Ndaki ametaka pia ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji ili mifugo isikae muda mrefu wakati wa kusafirishwa kwenda sokoni.

 

Awali akisoma ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Julius Mjengi amesema kabla ya tarehe 7 Novemba, 2020, mifugo iliyokuwa inatoka kwenye minada ya awali ya Handeni na Kilindi kuelekea nchini Kenya kupitia mpaka wa Horohoro haikuwa inafuata taratibu za forodha kama shehena nyingine.

 

Ameongeza kuwa takwimu za daftari la mifugo katika mpaka wa Horohoro zinaonyesha idadi ya mifugo iliyopitishwa kuelekea nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 17 kutoka mwaka 2003 hadi Novemba, 2020 ilikuwa ni ng’ombe 24,980 na Mbuzi na Kondoo 9,368 (sawa na wastani wa Ng’ombe 122 na Mbuzi/Kondoo 46 kwa mwezi).

 

Taarifa hiyo ilibainisha pia baada ya uchunguzi, ilionekana kuwa kati ya tarehe 7 Novemba, 2020 hadi tarehe 9 Desemba, 2020 (kipindi cha mwezi mmoja tu) jumla ya Ng’ombe 1,096 na Mbuzi na Kondoo 1,044 walipitishwa katika kituo cha Forodha kuelekea nchini Kenya, ambapo huo ni wastani wa idadi ya mifugo iliyopita mpakani ndani ya mwezi mmoja ukilinganisha na siku za nyuma.

 

Taarifa imebaini pia viashiria vya udanganyifu wa kurekodi idadi sahihi ya mifugo inayokaguliwa kwenda Kenya hususan katika mpaka wa Hororohoro – Tanga.

Baadhi ya wadau wa sekta ya mifugo, jeshi la polisi na wasimamizi wa mapato ya mifugo, wakati wa uwasilishwaji wa ripoti ya uchunguzi wa utoroshaji wa mifugo na mazao ya mifugo kwenda nchi za jirani ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza kuanzia leo kukamatwa kwa watuhumiwa 67 wa vitendo hivyo. Waziri Ndaki ametoa agizo hilo katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma. (26.01.2021)

Kamishna Msaidizi wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini Yusuph Sarungi, akisikiliza agizo la Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki la kumtaka kuanzia leo kuwakamata watuhumiwa 67 wa utoroshaji mifugo na mazao ya mifugo kwenda nchi za jirani. Waziri Ndaki ametoa agizo hilo katika ofisi za wizara hiyo zilizopo kwenye mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma, wakati wa uwasilishwaji wa ripoti ya uchunguzi wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake. (26.01.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wadau wa sekta ya mifugo, maafisa wa jeshi la polisi na wasimamizi wa mapato ya mifugo (hawapo pichani), wakati wa uwasilishwaji wa ripoti ya uchunguzi wa utoroshaji wa mifugo na mazao ya mifugo kwenda nchi za jirani na kuagiza kuanzia leo kukamatwa kwa watuhumiwa 67 wa vitendo hivyo. Waziri Ndaki ametoa agizo hilo katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma. (26.01.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel, akiweka kumbukumbu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wakati wa uwasilishwaji wa ripoti ya uchunguzi wa utoroshaji wa mifugo na mazao ya mifugo kwenda nchi za jirani. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo kwenye mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma. (26.01.2021)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni