Na Mbaraka Kambona, Kahama.
Wafugaji
na wafanyabiashara wa nguruwe na mazao yake wanaofanya shughuli zao Wilayani
Kahama, Mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua za haraka
kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Nguruwe ulioikumba wilaya hiyo na
kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kiuchumi.
Wafugaji
na wafanyabiashara hao walitoa ombi hilo Januari 26, 2021 wakati walipokuwa
wakiongea na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Profesa Hezron Nonga alipokwenda Wilayani Kahama kwa ajili ya kuongeza nguvu
kwa timu iliyoundwa na Serikali ya kudhibiti ugonjwa huo.
Wakiongea
kwa nyakati tofauti, wafugaji na Wafanyabiashara hao walisema kuwa tangu
ugonjwa huo uingie katika wilaya ya Kahama umesababisha hasara kubwa kwa
wafugaji na wafanyabiashara kwa sababu nguruwe wengi wamekufa huku biashara ya
mazao ya nguruwe hususan uuzaji wa nyama ukizorota kwa kiasi kikubwa.
Wilson
Sawa, Mmiliki wa Baa na Muuza nyama ya nguruwe wilayani Kahama alisema kuwa
biashara ya nyama ya nguruwe imekuwa ikisaidia biashara nyingine lakini tangu
kusitishwa kwa biashara hiyo baa nyingi ambazo zinauza nyama ya nguruwe
hazifanyi vizuri.
“Kusitishwa
kwa biashara hii kumeathiri uchumi wetu kwa sehemu kubwa, tunaiomba serikali
iharakishe kuudhibiti ugonjwa huu na iendelee kufanya tathimini ya maendeleo ya
ugonjwa ili kama unapungua waturuhusu tuendelee kufanya biashara,” alisema
Sawa.
Naye,
Pendo Emmanuel, mmliki wa bucha ya nyama ya nguruwe katika wilaya hiyo alisema
kabla ya ugonjwa huo kwa siku alikuwa anauza hadi kilo 80 kwa bei ya jumla na
rejareja lakini kwa sasa baada ya ugonjwa hakuna biashara anayoifanya.
“Kwa
kweli ugonjwa huu umeathiri kwa kiwango kikubwa katika kuendesha Maisha yangu,
siwezi kupeleka watoto shuleni, tunaiomba Serikali ione itakavyoweza kutusaidia
ili tuweze kuendesha maisha yetu,” alisema Emmanuel.
Frank
Kimaro, Mfugaji wa Nguruwe, Wilayani Kahama alisema kuwa kutokuwepo na sehemu
rasmi ya kuchinjia Nguruwe kumechangia kwa namna moja au nyingine katika
kusambaza ugonjwa huo kwa sababu wakati wote wamekuwa wakichinja nguruwe wao
katika maeneo yalipo mabanda yao.
“Ombi
langu kwa Serikali ituwekee sehemu itakayokuwa maalum kwa ajili ya kuchinja
nguruwe wetu hii itasaidia kudhibiti milipuko ya magonjwa lakini Serikali nayo
itapata mapato yake,”alisema Kimaro
Akizungumza
kuhusu hali halisi ya kuenea kwa ugonjwa huo wa homa ya nguruwe, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji, Kahama, Anderson Msumba alisema kuwa Serikali ipo kazini
kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa haraka ili shughuli za ufugaji na biashara
ya nguruwe na mazao yake ziweze kuendelea kama kawaida.
Aliongeza
kwa kusema kuwa tangu Serikali ilipoingilia kati sakata la ugonjwa huo kwa
kupeleka timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuungana na
wataalam wa Halmashauri idadi ya vifo imeanza kupungua na anaamini kwa juhudu
zinazoendelea ugonjwa huo sio muda mrefu utakoma.
“Nitoe
wito kwa wafugaji kuendelea kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalam ambayo
imewekwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kuhakikisha
mifugo yao haitoki nje ya mabanda yao, na wasiwe na tamaa, waache kuchinja
nguruwe wagonjwa kwa sababu atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa
dhidi yake,” alisisitiza Msumba.
Aidha,
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron
Nonga pamoja na kutoa elimu ya kina kuhusu hatua za kuchukua katika kudhibiti
ugonjwa huo usisambae, pia aliwataka wafugaji na wale wote wanaojihusisha na
biashara ya nguruwe kuzingatia masharti ya karantini iliyowekwa na Serikali na
atakayekaidi agizo hilo la Serikali sheria itachukua mkondo wake.
Alisema
kuwa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003 inazuia shughuli za
uchinjaji na usambazaji wa mifugo na mazao yake katika maeneo yenye mlipuko wa
magonjwa, na yeyote atakayekwenda kinyume na Sheria hiyo akibainika atapewa
adhabu ya papo kwa papo ya faini ya shilingi milioni tano (5) au akipelekwa
Mahakamani na kupatikana na hatia atahukumiwa adhabu yake ni kulipa faini ya
shilingi milioni kumi (10) au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za
Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (katikati waliokaa) akiwa
katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalam iliyoundwa na Serikali ya kudhibiti
mlipuko wa homa ya Nguruwe pamoja na Wafugaji na Wafanyabiashara wa Nguruwe na
mazao yake muda mfupi baada ya kufanya kikao cha kuwaelimisha wafugaji na
wafanyabiashara hao hatua za kuchukua ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae
zaidi. Kikao hicho kilifanyika Wilayani Kahama Januari 26, 2021.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji,
Kahama, Anderson Msumba (kulia) akiongea na Sehemu ya Timu ya Wataalam
iliyoundwa na Serikali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kwenda
kuungana na Wataalam wa Halmashauri kudhibiti mlipuko wa homa ya Nguruwe
ulioikumba Wilaya ya Kahama Januari 26, 2021.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za
Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga akimfanyia uchunguzi wa
Afya Nguruwe katika moja ya Mabanda yaliyopo Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga
Januari 25, 2021. Prof. Nonga alikwenda Wilayani humo kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa Timu
iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya
kudhibiti Mlipuko wa Ugonjwa wa homa ya Nguruwe uliyoikumba Wilaya ya Kahama.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kulia) akionesha damu iliyovilia katika
sikio la Nguruwe ikiwa ni moja ya kiashiria kuwa Nguruwe huyo ana homa kali
alipotembelea banda mojawapo la Mfugaji lililopo Wilayani Kahama, Mkoani
Shinyanga Januari 25, 2021. Kushoto ni Muhudumu wa Banda hilo Philipo Joseph.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kulia) akichukua namba ya simu ya
Mfugaji wa Nguruwe Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Stella Ngowi kwa ajili
ya kufanya ufuatiliaji wa hali ya Mifugo yake alipomtembelea nyumbani kwake
Januari 25, 2021.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga akiwakagua Nguruwe wadogo waliosongamana
sehemu mmoja wakiwa wanahisi baridi kali baada ya kupata homa kali katika banda
la mmoja wa wafugaji lililopo Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga Januari 25,
2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni