Na. Edward Kondela
Serikali imesema inatafuta
namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia tozo zote za mazao ya mifugo na uvuvi
pamoja na kuondoa tozo ambazo zinakwamisha sekta hizo zisikue.
Akizungumza jana (30.12.2020)
na baadhi ya wavuvi katika Kata ya Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani
Simiyu, wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo, Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema wizara itaangalia tozo ambazo zitakuwa rafiki
kwa wawekezaji, wafanyabiashara pamoja na wafugaji na wavuvi wa hali ya chini ili
kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinachangia kwa sehemu kubwa pato la
taifa.
“Tutaenda kuangalia ni tozo
zipi na baadhi tayari mmeshazitaja zikiwemo za kusafirisha mazao ya mifugo na
uvuvi nje ya nchi halafu tunatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia
hizi tozo zote.” Amesema Mhe. Ndaki
Waziri Ndaki ambaye
amefuatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul ameongeza kuwa
uwepo wa tozo ambazo zitakuwa rafiki katika kukuza sekta za mifugo na uvuvi
kutasababisha watu wengi kuwekeza katika sekta hizo na kuongeza pato la taifa
kwa kuwa shughuli za kuchumi zitaongezeka.
Kwa upande wake Naibu Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul ameendelea kusisitiza kuwa watu
wanaondelea kujihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja vitendo hivyo kwa kuwa
wizara haitafumbia macho ambao bado hawataki kuacha kuharibu mazao ya uvuvi
kupitia vitendo hivyo.
Amesema ni wakati sasa jamii
kushirikiana na serikali kuwabaini watu wanaojihusisha na uvuvi haramu kwa kuwa
wanaishi katika maeneo wanayofahamika ili serikali ichukue hatua na kwamba
Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazidi kutoa elimu juu ya athari ya uvuvi haramu kwa
jamii na taifa kwa ujumla.
Siku moja kabla ya kuanza
ziara ya kikazi Mkoani Simiyu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
wakati akihitimisha ziara ya siku mbili Mkoani Mwanza amefika katika Kijiji cha
Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu mkoani humo na kuzungumza na jamii ya
wavuvi na kuwasisitiza waanze kufuga samaki kupitia njia za vizimba na mabwawa
ili kujiongezea kipato na kuongeza kuwa mahitaji ya soko la samaki kwa sasa ni
makubwa.
Mhe. Ndaki amemuagiza Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah
kuhakikisha anaanzisha utaratibu wa kuwepo kwa kizimba cha mafunzo kwa ajili ya
kufugia samaki na kuhakikisha wataalamu kutoka wizarani wanafika katika kijiji
hicho kuwafundisha wananchi namna ya kufuga na kulisha samaki ili jamii ya hapo
iweze kupata mapato kupitia mazao ya uvuvi.
Waziri Ndaki amebainisha hayo
baada ya kutembelea vizimba vya kufugia samaki katika kijiji hicho
vinavyomilikiwa na Shamba la Konga na kufurahishwa na namna mwekezaji
anavyofuga samaki kwa wingi kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria kwa kuwa
ni sera ya serikali kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitano ajira zaidi ya
elfu arobaini na tano zinapatikana kupitia ufugaji wa samaki.
Katika kuhakikisha wananchi
wa Kijiji cha Kitongosima wananufaika kupitia ufugaji wa samaki Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bw. Lutengano Mwalwiba amewataka
wanakijiji hao kujiunga katika ushirika ili halmashauri hiyo iweze kuwakopesha
fedha kwa ajili ya shughuli za uvuvi huku Mwenyekiti wa Chama cha Wafuga Samaki
Ziwa Victoria Bw. Cyprian Matembo amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki kuangalia namna wizara inavyoweza kuwasaidia kupata vyakula vya
samaki kwa bei nafuu kwa kuwa kwa sasa vyakula vingi vimekuwa vikiagizwa kutoka
nje ya nchi na kuongeza gharama za uzalishaji.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki leo (31.12.2020) anahitimisha ziara ya kikazi katika mikoa
mitatu ya Kanda ya Ziwa kwenye Mkoa wa Shinyanga, baada ya kufanya ziara kwenye
mikoa ya Mwanza na Simiyu, akiambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe.
Pauline Gekul.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akifuatiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul wakipatiwa maelezo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, namna ya kufuga samaki kwa njia ya vizimba wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Ndaki katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, kujionea namna mwekezaji Shamba la Konga anavyofuga samaki kupitia vizimba ndani ya Ziwa Victoria. (31.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wavuvi katika Kata ya Nyamikoma,
iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, wakati wa ziara yake ya siku moja
mkoani humo, na kubainisha kuwa serikali inatafuta namna ya kuwa na kituo
kimoja cha kulipia tozo zote za mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na kuondoa tozo
ambazo zinakwamisha sekta hizo zisikue na kuainisha tozo ambazo zitakuwa rafiki
katika kuzifanya sekta hizo kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
(31.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akishuhudia na kuhesabu idadi ya vizimba vya kufugia samaki
vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya
ya Magu Mkoani Mwanza, ambavyo vinamilikiwa na Shamba la Konga na kuwataka
wananchi wa kijiji hicho kuanza kufuga samaki ili wajiongeze kipato kwa kuwa
mahitaji ya soko la samaki yanayongezeka na kutaka kuanzishwa kwa vizimba vya
mafunzo katika kijiji hicho kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (31.12.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akizungumza na baadhi ya wavuvi katika Kata ya
Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu akiwataka watu wanaondelea
kujihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja vitendo hivyo na kubainisha ni
wakati sasa jamii kushirikiana na serikali kuwabaini watu wanaojihusisha na
uvuvi haramu kwa kuwa wanaishi katika maeneo wanayofahamika ili serikali
ichukue hatua. (31.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni