Nav bar

Jumamosi, 2 Januari 2021

HALMASHAURI ZAONYWA WAFANYABIASHARA KUCHANJA MIFUGO, MIKATABA YAO KUVUNJWA

Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amepiga marufuku halmashauri zote nchini kutotumia wafanyabiashara kuchanja mifugo na kutaka kuvunjwa kwa mikataba hiyo mara moja.

 

Waziri Ndaki amebainisha hayo jana (31.12.2020) alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Shinyanga ambapo alipokuwa katika josho la kuogeshea mifugo la Kijiji cha Mipa kilichopo Wilaya ya Kishapu mkoani humo kwa ajili ya kushuhudia uogeshaji mifugo na utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, wafugaji wamemlalamikia kuwa baadhi ya ng’ombe kijijini hapo wamekuwa wakivimba na wengine kufa baada ya kupatiwa chanjo.

 

Waziri Ndaki akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema kuanzia sasa chanjo zote nchini zitatolewa na wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa na kugoma kushuhudia zoezi la uchanjaji lililokuwa limeandaliwa baada ya kukasirishwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kutokuwa na takwimu yoyote ya idadi ya ng’ombe waliovimba na wengine kufa baada ya kuchanjwa.

 

“Halmashauri zetu zote kuanzia sasa hivi ni marufuku kutumia wafanyabiashara kuchanja mifugo yetu, halmashauri zitumie wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa waweze kuchanja mifugo ya wananchi wetu, hao wafanyabiashara kama mmeingia mikataba nao hiyo mikataba ivunjeni haraka iwezekanavyo hatuwezi kuchezea akili za watu namna hii hatuwezi kutuma wafanyabiashara waende kuchanja ng’ombe wanavimba na wanakufa halafu taarifa hatuna.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Aidha, Waziri Ndaki katika ziara yake ya siku moja Mkoani Shinyanga amefika katika mnada wa upili wa Mhunze ambao ni moja ya minada inayosimamiwa na wizara na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kumuondoa mara moja kazini mhasibu wa halmashauri hiyo anayefanya kazi katika mnada huo Bw. Athanas Msiba kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu katika kuandika idadi ya mifugo inayoingia na kutoka katika mnada huo hali inayosababisha wizara na halmashauri kukosa mapato stahiki.

 

“Mkurugenzi huyu Athanas Msiba siyo mwaminifu hafai kukaa hapa tena aondoke sasa hivi ulete mtu mwingine, watu wakipita hapa na mbuzi watano anaandika watatu anaandika kidogo hafai aondoke hapa.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bw. Emmanuel Johnson amesema amepokea maelekezo hayo na atayafanyia kazi kwa kuihusisha pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili ifanye ufuatiliaji kwa kuwa serikali haiko tayari kuwa na watu wenye tabia ya namna hiyo.

 

Akiwa katika mnada huo Waziri Ndaki amepata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wafugaji ikiwemo ya kuzuiwa kuondoa mifugo mnadani kabla ya saa 12 jioni hali inayohatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa fisi wengi kwenye maeneo ya mashamba wakati wa kurudi nyumbani majira ya jioni hali iliyomlazimu Waziri Ndaki kuutaka uongozi wa mnada utafute utaratibu wa kuwaruhusu wafanyabiashara kuondoka kabla ya muda huo wakiwa wamemaliza shughuli zao.

 

“Mtu amemaliza biashara yake mkagueni vizuri kwenye mlango wa kutokea aende zake akimaliza hapa akikaa saa mbili aondoke, akikaa dakika 15 aondoke ili mradi amemaliza shughuli zake siyo unawaleta unawafungia humu haka kamekuwa kajela kadogo? Hapana hiyo.” Amefafanua Waziri Ndaki

 

Akiwa Mkoani Shinyanga Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul, ametembelea ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa yaliyopo katika Manispaa ya Shinyanga unaogharimu Shilingi Bilioni 5.5 ambapo tayari zimelipwa Shilingi Bilioni 5.1 na umefikia asilimia 97 hadi kukamilika kwake.

 

Mara baada ya kukamilika machinjio hayo Mwezi Februari Mwaka 2021, yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 mbuzi na kondoo 1,000 kwa siku.

 

Siku moja kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Shinyanga, Waziri Ndaki akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul walifika katika shamba la mifugo la serikali Shishiyu Holding Ground lililopo katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, ambapo Waziri Ndaki amesema shamba hilo lenye ekari 10,240 halina tija kwa sasa kwa kuwa limebaki pori na hakuna mifugo.

 

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inataka maeneo yote ya mashamba ya serikali ya mifugo ambayo yapo chini ya wizara kuyaweka chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), ili NARCO washughulike nayo kwa sababu ni chombo pekee cha wizara kinachokubaliwa kufanya biashara ya kupangisha maeneo kwenye mashamba ya wizara.

 

Waziri Ndaki amefikia hatua hiyo baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuomba ekari 1,500 ili kuendeleza shamba hilo kwa ajili ya kunenepesha mifugo ikiwemo kuotesha malisho pamoja na kuelimisha wananchi namna ya kufuga mbegu bora za mifugo, ambapo Waziri Ndaki amesema atatoa maamuzi ya ombi lao haraka iwezekanavyo.

 

Amefafanua kuwa haina maana wizara kuwa na maeneo makubwa katika mashamba yake ambayo hayatumiki huku wafugaji wakiwa hawana maeneo ya malisho yao hivyo ni bora kuyapangisha ili serikali iweze kupata mapato kupitia mashamba hayo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul na baadhi ya viongozi kutoka wizarani na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, alipokuwa akikagua miundombinu ya mnada wa upili wa Mhunze ambao ni moja ya minada inayosimamiwa na wizara alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo. (31.12.2020)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul katika josho la Kijiji cha Mipa kilichopo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga ambapo amegoma kushuhudia zoezi la utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, kufuatia taarifa kutoka kwa baadhi ya wafugaji kuwa mifugo imekuwa ikivimba na mingine kufa baada ya kupatiwa chanjo hali iliyomlazimu kupiga marufuku halmashauri zote nchini kutotumia wafanyabiashara kuchanja mifugo na kuvunja mikataba yao mara moja. (31.12.2020)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akimuonya mhasibu wa mnada wa upili wa Mhunze uliopo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Bw. Athanas Msiba kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu katika kuandika idadi ya mifugo inayoingia na kutoka mnadani hapo na kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kumuondoa Bw. Msiba katika mnada huo mara moja na kumpeleka mhasibu mwingine. (31.12.2020)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akipatiwa maelezo ya utendaji kazi wa moja ya mashine ya kuchuna ngozi ya ng’ombe na meneja mradi wa machinjio ya kisasa ya Manispaa ya Shinyanga Bw. Veran Mwaluko, mara baada ya Waziri Ndaki kufanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo na kufika katika machinjio hayo yanayotarajiwa kukamilika Mwezi Februari Mwaka 2021 ambapo yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 na mbuzi na kondoo 1,000 kwa siku. (31.12.2020)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni