Na. Edward Kondela
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wakurugenzi wa halmashauri
zenye masoko ya samaki ya kimataifa kuacha kupanga tozo za mazao ya uvuvi bila
kuwasiliana na wizara hiyo ili kuondoa kero za tozo zinazowakumba wananchi
wanaofanya biashara katika maeneo hayo.
Akizungumza
jana (03.01.2021) mara baada ya kutembelea mnada wa mifugo uliyopo Kijiji cha
Buzirayombo Kata ya Bukome na soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha
Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, Waziri Ndaki amesema
wizara haitaki kusikia kero za wafanyabiashara kuhusu tozo zisizo rafiki katika
masoko hayo likiwemo soko la samaki la kimataifa la Kata ya Kirumba lililopo
Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.
“Kuhusiana
na tozo niseme tu kwa wakurugenzi walio na masoko haya ya kimataifa kwa maana
ya soko la Kirumba na Kasenda, sisi wizara hatutaki kusikia kelele katika haya
masoko mnapopanga tozo zenu hakikisheni kwa masoko haya mawili tuwasiliane ili
tupange tozo za kwenu na kwetu ambazo zitakuwa rafiki.” Amesema Mhe. Ndaki
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani amemuomba Waziri
Ndaki kupitia vikundi vya wavuvi vilivyosajiliwa, wizara ione namna ya
kuwasaidia wavuvi mikopo yenye riba nafuu pamoja na kuwanunulia nyavu ili
kuacha kujihusha na uvuvi usiofuata utaratibu.
Nao
baadhi ya wavuvi na wananchi wanaofanya shughuli za kibiashara katika soko la
samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda wamesema wanashirikiana na
serikali kuhakikisha wanadhibiti uvuvi haramu.
Aidha,
wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi namna inavyofanya jitihada za
kuhakikisha inaboresha mazingira ya wavuvi ili sekta ya uvuvi iweze kuwa na
tija kwa wadau wa sekta hiyo na hatimaye waweze kunufaika kiuchumi.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekagua pia ujenzi wa machinjio ya
kisasa yanayojengwa katika eneo la mnada wa mifugo Kijiji cha Buzirayombo Kata
ya Bukome, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika
ofisi za soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya
Muganza, Wilaya ya Chato Mkoani Geita. Ofisi hizo zinatumika pia kama kituo kwa
ajili ya kudhibiti uvuvi haramu. (03.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt.
Medard Kalemani (wa kwanza kulia) pamoja na viongozi wengine wa serikali wakati
akikagua shughuli mbalimbali zinazoendelea katika soko la samaki la kimataifa
lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
(03.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa soko la samaki la
kimataifa Bw. Suleiman Said (wa pili kushoto) mara baada ya Waziri Ndaki
kutembelea soko hilo lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya
Chato Mkoani Geita. (03.01.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni