Na Mbaraka Kambona,
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amesema kuwa hakuna haja ya kuendelea
kuwa na Maafisa Uvuvi ambao wanashirikiana na wahalifu kufanya vitendo vya
hujuma wakati kuna vijana wengi wenye nia njema ya kulitumikia Taifa
wanahangaika na ajira.
Gekul
aliyasema hayo alipotembelea Kiwanda cha kuchakata samaki, Alpha kilichopo
Vingunguti jijini Dar es Salaam Januari 5, 2021.
Kwa
mujibu wa Gekul sehemu kubwa ya upungufu wa rasilimali za uvuvi unachangiwa na
baadhi ya Maafisa Uvuvi ambao sio waaminifu ambao wamekuwa wakishirikiana na
wahalifu kufanya uvuvi usioendelevu unaopelekea kupungua kwa samaki.
“Tulikuwa
Kanda ya ziwa, na hapa pia kilio ni hicho hicho malighafi, malighafi zinapungua
kwa sababu baadhi ya maafisa uvuvi wanashiriki katika vitendo vya uvuvi haramu,
wanashirikiana na wahalifu, hata pale ambapo vyombo vya ulinzi na usalama
vinapotaka kufanya operesheni ya kuwakamata wahalifu wamekuwa wakitoa taarifa
kwa wahalifu hao kama ambavyo ilitokea hivi karibuni kule Wilayani
Babati,”alisema Gekul
“Kwa
nini tuendelee na watu wa namna hii wakati kuna vijana wengi wenye nia njema na
taifa lao wapo huko nje hawana ajira na huku ndani ya serikali kuna baadhi ya
watu wanahujumu taifa na uchumi wa nchi, hatuna haja kuendelea kuwa na watu
kama hawa,” alisisitiza Gekul
Aliendelea
kusema kuwa itakuwa aibu wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza hapa nchini halafu
washindwe kuendelea na uzalishaji kwa kukosa malighafi kutokana na kushindwa
kudhibiti uvuvi haramu.
Aliongeza
kuwa wawekezaji ni muhimu kwa uchumi wa taifa kwa sababu wanalipa kodi na tozo
mbalimbali ambazo zinasaidia kukuza pato la taifa, uchumi wa nchi na kutoa
ajira kwa vijana.
Aidha,
aliwataka maafisa hao ambao wanaojihusisha na vitendo hivyo kujirekebisha na
washirikiane kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kwa pamoja waweze
kukomesha vitendo hivyo kwa lengo la kunusuru rasilimali za uvuvi.
“Tutimize
wajibu wetu tukijuwa kuwa uvuvi haramu ukiendelea tutaviua hivi viwanda na
matokeo yake ajira nazo kwa vijana wetu zitapotea,” alieleza Gekul
Gekul
aliwataka maafisa uvuvi wote nchini kuendelea kuchukua hatua za haraka
kudhibiti hali iliyopo ya upotevu wa rasilimali za uvuvi katika maeneo yote
yalipo maji na maziwa.
Awali, Meneja wa Uzalishaji wa Kiwanda cha Alpha, Sreejish Srinivasan wakati akitoa taarifa ya uzalishaji wa kiwanda hicho alieleza kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uchache wa malighafi kwa ajili ya kuchakatwa kiwandani hapo na mpaka sasa wanafanya shughuli zao chini ya asilimia 15 ya uwezo wa kiwanda hicho.
Wafanyakazi wa Kiwanda cha
kuchakata Samaki, Alpha wakimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline
Gekul (wa kwanza kulia) Minofu ya Samaki aina ya Pweza ambayo imechakatwa
katika Kiwandani hicho kilichopo jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri
alikitembelea kiwanda hicho Januari 5, 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Pauline Gekul (wakwanza kushoto) akiwaeleza jambo Wanafunzi wa Chuo cha
Mafunzo ya Mifugo (LITA) alipotembelea maabara wanayoitumia wanafunzi hao
kuchunguza magonjwa ya mifugo kilichopo jijini Dar es Salaam Januari 5, 2021.
Katikati ni Mtendaji Mkuu, Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt.
Pius Mwambene.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Pauline Gekul akikagua moja ya nyavu inayozalishwa katika Kiwanda cha
kutengeneza nyavu za kuvulia Samaki, Nyamagara kilichopo Chanika, jijini Dar es
Salaam alipokitembelea Januari 5, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni