Wataalamu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA)
wametakiwa kuzingatia mafunzo wanayopatiwa ili wazalishaji wa vyakula vya
mifugo waweze kuzalisha vyakula vyenye ubora unaotakiwa.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo
jana (06.01.2021) wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya ukaguzi wa
rasilimali ya vyakula vya mifugo yanayofanyika jijini Dar es Salaam na
kubainisha kuwa wataalamu wataweza pia kutekeleza majukumu mapya ya kuzingatia
zaidi ubora wa vyakula vya mifugo.
"Uwepo wenu kama wakaguzi utarahisisha huduma kwa wananchi,
na upatikanaji kwa sampuli zaidi ili kupata uhakika wa ubora wa vyakula vya
mifugo nchini" alisema Dkt. Bitanyi.
Aidha, Dkt. Bitanyi ameishukuru timu wa wataalamu wa idara ya
uendelezaji wa malisho na masilimali za vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na afisa mifugo mtafiti mkuu
kutoka TVLA kwa namna wanavyoshirikiana katika mafunzo hayo ambayo yanalenga
kuboresha zaidi uwepo wa vyakula bora vya mifugo.
"Ni matarajio ya wakala kuwa kupitia mafunzo haya mtaongeza
ufanisi katika kazi zenu pia kuongeza uwezo wa wakala katika jukumu zima la
udhibiti wa uzalishaji holela wa vyakula vya mifugo na kuwezesha kuongeza tija
katika sekta ya mifugo." Alisema Dkt. Bitanyi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi alisema mafunzo
hayo ya siku tatu yatawawezesha wataalamu kufahamu sheria na kanuni za ukaguzi
wa vyakula vya mifugo, uzalishaji sahihi wa vyakula vya mifugo, weledi katika
kuchambua ubora wa rasilimali za vyakula vya mifugo wakati wa ukaguzi, ukaguzi
wa maeneo ya utunzaji wa vyakula vya mifugo na namna bora ya uchakataji wa
sampuli.
Pia, amewasihi wataalamu kutumia muda uliopo kwenye mafunzo hayo
kuhakikisha wanazingatia wanayofundishwa na kuweka katika mipango yao ya kazi
hasa kutokana na ukweli kuwa, TVLA imeanzishwa ikiwa na majukumu ya kuchunguza
magonjwa ya mifugo, uhakiki ubora wa vyakula vya mifugo, upimaji wa nguvu ya
dawa za kuogeshea pamoja na uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ilianzishwa
chini ya Sheria ya Wakala za Serikali ya Mwaka 2012 kwa lengo la kutoa huduma
za uchunguzi, utambuzi na utafiti wa magonjwa, vimelea vya magonjwa ya wanyama
na ubora wa bidhaa za mifugo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akieleza
lengo na majukumu ya wataalamu (hawapo pichani) wakati wa kufungua mafunzo
ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo yanayoendelea jijini Dar es
salaam. (06.01.2021)
Mkurugenzi wa Utawala
na Biashara kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Richard
Masanja akiwasisitiza wataalamu kuzingatia yote wanayofundishwa kabla ya
kumkaribisha Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi kufungua
mafunzo hayo jijini Dar es salaam. (06.01.2021)*
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia kwa makini maelezo ya Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinary Tanzania (TVLA), Bi. Wende Maulaga wakati akitoa mafunzo hayo kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. (06.01.2021)*
Timu ya wataalam
wanaotoa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo, (kushoto juu)
ni Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Idara ya
Uzalishaji Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Bw. Rogers Shengoto,
Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu Bi. Wende Maulaga (kulia) na Afisa
Mifugo kitengo cha Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bi. Theodata Salemma
wakitoa elimu kwa baadhi ya washiriki wa mafunzo jijini Dar es salaam.
(06.01.2021)*
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania ( TVLA), Dkt. Stella Bitanyi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakurugenzi pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tatu ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. (06.01.2021)*
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni