Nav bar

Alhamisi, 7 Januari 2021

VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA UFUGAJI SAMAKI KATIKA MABWAWA

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewahimiza vijana kujihusisha na ufugaji wa samaki katika mabwawa huku akisema fursa hiyo itawaokoa vijana wengi kuondokana na kilio cha ukosefu wa ajira nchini.

 

Gekul aliyasema hayo alipotembelea Kampuni ya ufugaji wa Samaki inayojulikana kwa jina la Bigfish iliyopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021.

 

Alisema kuwa muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa samaki katika mabwawa kwasababu uvuvi wa kutegemea maji ya asili umekuwa mkubwa na kupelekea kupungua kwa rasilimali za uvuvi, hivyo kimbilio pekee ambalo litawawezesha vijana wengi kupata ajira ni ufugaji wa samaki katika mabwawa.

 

Aliongeza kuwa Serikali ipo mbioni kuweka miongozo na kanuni za ufugaji huo ili kuwalinda na kuwawezesha wafugaji waweze kufuga vizuri na kwa kuzingatia taratibu zitakazowekwa.

 

“Serikali itawawezesha vijana kwa hali ya juu, kuwajengea mabwawa, kuwapatia mafunzo ya ufugaji bora wa samaki ili vijana wetu waweze kujikwamua na suala la ukosefu wa ajira,” alisema Gekul

 

Aliendelea kusema kuwa Rais, Dkt. John Magufuli aliahidi ajira zaidi ya milioni 8, moja ya sekta ambayo inategemewa kutengeneza ajira hizo ni ya uvuvi hivyo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujikomboa kiuchumi.

 

Kuhusu uwezeshaji, Gekul aliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 10 katika mapato yao kwa ajili ya kuwawezesha vijana na watu wenye Ulemavu ili waweze kufanya ufugaji katika mabwawa na kujipatia ajira.

Aidha, Gekul alisema kuwa anafahamu changamoto zinazokabili ufugaji wa samaki wa mabwawa ni pamoja na uhaba wa vifaranga vya samaki na ukosefu wa chakula cha kutosha na cha uhakika kwa ajili ya samaki hivyo alitumia fursa hiyo kuiagiza Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kutafuta muarobaini wa changamoto hizo ili kuwaondolea kero hiyo wafugaji.

 

Aliongeza kuwa ufugaji wa samaki katika mabwawa utasaidia kupunguza kilio cha uhaba wa malighafi unaokabili viwanda vingi nchini huku akiongeza kuwa ufugaji huo pia utasaidia kupunguza uvuvi haramu kwa sababu watu watakuwa na chanzo mbadala cha kujipatia kipato.


Kaimu Meneja Mkuu, Shirika la Uvuvi (TAFICO), Ester Mulyila (kulia) akimpokea Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea Shirika hilo lililopo jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. 

Mshauri wa Uvuvi kutoka Japan, Koji Hase (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul(kulia) baadhi ya taarifa kuhusu uvuvi alipotembelea Shirika la Uvuvi la Tanzania (TAFICO) lililopo jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. 

Afisa Uzalishaji Vifaranga, Kampuni ya Bigfish, Pastory Aloyce (kushoto) akifafanua jambo kuhusu ufugaji wa samaki kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea eneo la ufugaji wa samaki la kampuni hiyo iliyopo Wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. 

Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimerei (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Mradi wa SWIOFish, Dkt. Nichrous Mlalila. 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni