Na. Edward Kondela
Wafugaji wametakiwa kuanza
kufikiria kuwa na ng’ombe bora badala ya kuwa na ng’ombe wengi wasio na ubora
ambao hawakidhi tija katika maisha yao kwa kutotoa mazao bora ambayo hayawezi
kutoa kipato cha kuridhisha.
Akizungumza jana (29.12.2020)
katika Kijiji cha Kinango kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wakati
akishuhudia zoezi la uogeshaji mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali wakati wa
ziara yake ya siku mbili mkoani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki amesema mifugo mingi wakiwemo ng’ombe ni njia mojawapo ya kutunza fedha
ambayo imekuwa ikitumiwa na wafugaji hivyo ni muhimu wafugaji hao kuhakikisha
mifugo yao inakuwa bora kwa kuipatia huduma muhimu ikiwemo ya kuiogesha.
“Nchi yetu tuna ng’ombe wengi
sana, lakini wengi siyo bora kama inavyotakiwa sasa tunatakiwa kutoka kuwa na
ng’ombe wengi tu bali tuwe na ng’ombe walio bora, tukiwa na ng’ombe wengi wasio
bora hawatusaidii sana katika maisha yetu, kwa sababu lengo la kuwa na ng’ombe
atupe nyama, atupe maziwa na atupe kipato sasa tufikirie kuwa na ng’ombe bora
na moja ya njia ya kuwa na ng’ombe bora ni hii ya kuwaogesha.” Amesema Mhe.
Ndaki
Mhe. Ndaki ameongeza kuwa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa fedha 2020/2021 imetenga bajeti ya
kukarabati majosho kadhaa yaliyopo maeneo mbalimbali nchini na kuahidi kuwa
wizara itakarabati majosho matano yaliyopo katika Wilaya ya Magu ili mifugo
mingi iweze kuogeshwa na kuwa bora.
Pia, Mhe. Ndaki akiwa
ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul katika ziara
hiyo amesema njia nyingine ya kuwa na ng’ombe bora ni wafugaji kuhakikisha
mifugo yao inapata malisho bora ambayo yatafanya mifugo hiyo kuwa na afya bora
lakini kwa sasa wafugaji wamekuwa wakichunga katika maeneo machache hali
inayofanya mifugo kutokula chakula kinachotakiwa.
Ameongeza kuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imekuwa ikishughulikia sana suala la malisho ambalo ni moja ya
tatizo kubwa kwa wafugaji pamoja na maji na kutumia fursa hiyo kumshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kutokana na kuruhusu
wafugaji wachunge kwenye baadhi ya maeneo yaliyokuwa ya hifadhi na mengine
kuzuiliwa hali iliyotoa ahueni kwa wizara kupata maeneo ya kulisha mifugo ili
iwe na ubora.
Kwa upande wake Kaimu Msajili
wa Bodi ya Nyama Nchini (TMB) Bw. Iman Sichalwe amewaeleza wafugaji kuwa suala
la kuogesha mifugo dhidi ya magonjwa ni muhimu kwa kuwa limekuwa likizuia
Tanzania kuuza nyama katika nchi mbalimbali kutokana na viwanda vya kuchinja na
kuchakata nyama kutopata mifugo bora.
Amefafanua kuwa uogeshaji
unaboresha afya ya mfugo ikiwemo ya nyama na ngozi hivyo kuvifanya viwanda
kufanya kazi na kuwaongezea vipato wananchi kwa kupata masoko ya kuuza mifugo
yao, serikali kupata fedha kupitia tozo mbalimbali, upatikanaji wa fedha za
kigeni na kwamba hali hiyo haitawezekana endapo mifugo haitadhibitiwa na
magonjwa ili kupata nyama bora na kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi bora.
Katika ziara hiyo ya siku
mbili Mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametembelea
pia kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha Alpha Choice kilichopo wilayani
Magu na kuzungumza na baadhi ya wafugaji waliofika kiwandani hapo kwa kuwataka
waanze kubadilisha ubora wa mifugo yao kwa kuwachanja, kuwaogesha, kuwapatia
maji na malisho yanayotosheleza na kuacha kuwachunga katika maeneo marefu ili
mifugo hiyo iwe na afya nzuri ambayo mfugaji atauza kwa bei nzuri na mwenye
kiwanda kupata mfugo wenye mazao bora.
Mhe. Ndaki amesisitiza hilo
baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wawekezaji kwenye viwanda vya
kuchinja na kuchakata nyama kutopata ng’ombe bora ambao wanaweza kukidhi katika
soko la kimataifa hali ambayo wakati mwingine nyama kukataliwa na baadhi ya
nchi kutokana na mifugo kuwa na magonjwa na nyama kutokuwa na ubora unaotakiwa.
“Nawaombeni sana tuanze
kuboresha ng’ombe wetu ili tupate faida ya kuwa na kiwanda hapa na kingine
nimekiona kule wilayani Misungwi na chenyewe wanapata ng’ombe kidogo sababu ni
hiyo hiyo ng’ombe wetu hawajawa bora sana, sasa wawekezaji hawa wamelazimika
wawe wananununa ng’ombe wanawafuga mahali kwanza wanawalisha ili wabadilike
sura na afya waliyotoka nayo kwa wafugaji ambao
ni sisi.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akiambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline
Gekul na Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah pamoja na
wataalam wengine kutoka wizarani, amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili
Mkoani Mwanza ambapo amejionea mambo mbalimbali yanayohusu sekta za mifugo na
uvuvi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa zoezi la kuogesha mifugo lililofanyika katika josho la Kijiji cha Kinango kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, wakati Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo. (29.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul (anayemfuata) wakishuhudia nyama iliyochakatwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi baada ya kufanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama Alpha Choice kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. (29.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wafugaji (hawapo pichani)
waliofika katika kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama Alpha Choice kilichopo
Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, ambapo amewataka wabadili fikra za ufugaji na
wafuge kisasa ili wapate ng’ombe bora. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul na kulia kwake ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah. Waziri Ndaki amemaliza ziara ya
kikazi ya siku mbili Mkoani Mwanza. (29.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni