Jumatatu, 30 Novemba 2020
WAFUGAJI NA WAKULIMA KUNUFAIKA KUPITIA KIWANDA CHA NYAMA NGURU HILLS
Serikali imesema katika kuboresha na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro, inasisitiza uwepo wa miradi ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa makundi yote mawili.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabriel amesema hayo (28.11.2020) katika Wilaya ya Mvomero Mkoani
Morogoro alipotembelea ujenzi wa mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya
Nguru Hills na kubainisha kuwa mradi huo unaotarajia kukamilika mwezi Aprili
Mwaka 2021 utakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji na wakazi wa Mkoa wa
Morogoro.
“Tumekuja kuangalia shughuli zinazoendelea kutokana na kikao ambacho
tulikuwa nacho katika ofisi ya katibu tawala wa mkoa na mkuu wa Mkoa wa
Morogoro katika kuboresha shughuli za mifugo kwenye mkoa huo na kuondoa
changamoto za migogoro ya wafugaji ambapo uongozi wa mkoa waliniambia juu ya
mradi huu ambao utakuwa na msaada mkubwa sana kwa wakulima na wafugaji wa mkoa
wa Morogoro na nchi kwa ujumla.” Amesema Prof. Gabriel.
Prof. Gabriel amebainisha kuwa mradi huo wa kipekee ambao mara baada ya
kiwanda hicho kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe zaidi ya 200 na
mbuzi zaidi ya 1,000 kwa siku, kumejengwa mabwawa makubwa ambayo yatakuwa
yanakusanya maji yanayotoka kwenye machinjio, kisha kutibiwa kabla ya kutumika
tena kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
“Mradi huu una jambo mahsusi kuliko mingine, maji haya ya mabwawa
yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji huu ni moja kati ya miradi ambapo wafugaji
na wakulima watanufaika ili wote waone huu mradi ni wa kwao kwa ajili ya uchumi
wetu.” Ameongeza Prof. Gabriel.
Aidha, amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 25,
ambao unashirikisha wabia mbalimbali ukiwemo Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa
Umma (PSSSF), ni azma ya serikali katika kuzidi kuboresha mazingira ya
uwekezaji hapa nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mifugo hivyo
kuwataka wafugaji kuboresha mifugo yao kwa kufuga ng’ombe bora wa kisasa na
kupitia miradi ya kunenepesha mifugo ili waweze kuuza mifugo yenye ubora katika
viwanda vya kusindika mazao ya mifugo hapa nchini ili sekta izidi kukua na
kuchangia pato la taifa kupitia uchumi wa viwanda.
Pia katibu mkuu huyo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya
jitihada mbalimbali za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo mingi na bora kwa
kuhakikisha mifugo inaogeshwa ili kujikinga dhidi ya magonjwa na kuwataka
wakurugenzi wa halmashauri kote nchini, kuhakikisha maeneo yao yana majosho ya
kutosha kwa ajili ya kuogeshea mifugo na kuwataka wayafanyie ukarabati majosho
ambayo hayafanyi kazi.
“Tufuge kisasa Namibia, Botswana wana ng’ombe wachache lakini wanauza
kwa wingi nyama nje ya nchi, ndiyo maana tunaimarisha afya za mifugo, ndiyo
maana nchi nzima tunashughulika na masuala ya uogeshaji niwatake wakurugenzi wa
halmashauri wahakikishe kwenye maeneo yao kuna majosho ya kutosha na niwatake
yale ambayo hayafanyi kazi vizuri yaboreshwe. Ameongeza Prof. Gabriel.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabriel amelitaka pia Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya
wizara hiyo pamoja na Idara ya Uzalishaji na Masoko kwa kushirikiana na PSSSF
kukutana haraka ili kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mradi
wa kiwanda cha nyama Nguru Hills ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero
Bw. Hassan Chama Hassan amemwambia katibu mkuu huyo kuwa, mradi huo ukikamilika
kwa wakati wafugaji watanufaika kwa kuwa wanakabiliana na changamoto ya kuuza
mifugo yao kupitia minada ambapo wanakutana na madalali ambao wanafanya bei za
mifugo kuwa chini, huku Meneja Ujenzi wa mradi huo kutoka PSSSF Mhandisi
Grayson Bambaza akibainisha kuwa wafugaji watakuwa wanauza mifugo yao kwa kilo
na siyo kwa kukadiria kulingana na umbo la mfugo.
Mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills unaotarajia
kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021, unategemewa kutoa ajira kwa wafanyakazi 120
hadi 200 kulingana na uzalishaji.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto)
akizungumza na baadhi ya viongozi wa Ranchi ya Nguru Hills juu ya mradi wa
kiwanda cha nyama kinachojengwa katika ranchi hiyo huku akiwataka wahakikishe
mara baada ya kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi, kitoe bidhaa bora ili
kushindana na soko la kimataifa. Meneja Mkuu wa ranchi hiyo Bw. Paul Phillips
(aliyesimama katikati) amemuhakikishia katibu mkuu huyo kuzingatia maelekezo
yake. (28.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mabwawa
yanayojengwa katika Ranchi ya Nguru Hills, ambayo yatapokea maji yatakayokuwa
yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha
umwagiliaji. Prof. Gabriel ameambatana na viongozi wa ranchi, viongozi wa
halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na baadhi ya watumishi kutoka wizarani.
(28.11.2020)
Muonekano wa moja ya mabwawa
yanayojengwa katika Ranchi ya Nguru Hills, ambayo yatapokea maji yatakayokuwa
yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha
umwagiliaji. (28.11.2020)
Muonekano wa nje wa ujenzi wa
kiwanda cha nyama Nguru Hills kinachotarajiwa kutoa ajira kati ya wafanyakazi
120 hadi 200 kulingana na uzalishaji. (28.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua ujenzi wa
kiwanda cha nyama Nguru Hills huku akijihakikishia vipimo vilivyobainishwa
katika mchoro wa jengo hilo. (28.11.2020)
Muonekano wa moja ya maeneo
ya ndani ya kiwanda cha nyama Nguru Hills kitakachokuwa na uwezo wa kuchinja
mbuzi zaidi ya 200 na ng’ombe zaidi ya 1,000 kwa siku. (28.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha
ya pamoja na viongozi wa Ranchi ya Nguru Hills viongozi kutoka halmashauri ya
Wilaya ya Mvomero na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (28.11.2020)
Jumamosi, 28 Novemba 2020
WAFUGAJI WASHAURIWA KUWEKEZA KATIKA KILIMO CHA MALISHO.
WAFUGAJI WASHAURIWA KUWEKEZA KATIKA KILIMO CHA MALISHO
Wafugaji wa Ng’ombe wameshauriwa
kujikita katika kilimo cha Malisho ili wawe na uhakika wa malisho bora kwa
ajili ya mifugo yao na kuachana na uchungaji wa kutafuta malisho.
Mtendaji Mkuu wa Shamba la Ndoto,
Hartmut Rottcher aliyasema hayo kwa Wakurugenzi na Mameneja wa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi waliotembelea shamba la mfano la Ndoto lililopo Mkoani Iringa Novemba
27, 2020.
Rottcher alisema kilimo cha malisho
yaliyo bora kinasaidia kuwapatia mifugo uhakika wa chakula bora huku akieleza
kuwa mifugo ni muhimu kupewa pumba kwa kiasi na sio kuzidisha kwani
kufanya hivyo hupelekea ng’ombe kupata asidi tumboni na kuuwa bakteria ambao
husaidia kukata kata majani tumboni kwa mnyama.
Alisema kuwa yeye anafanya kilimo
cha malisho kwa kumwagilia na ametenga maeneo katika mashamba yake illi
kusaidia kulisha mifugo kwa mzunguko na kuipatia mifugo mahitaji
wanayotaka na sio kuletewa chakula kwenye maboma yao.
“Njia ya kulisha kwa mzunguko
husaidia kupata muda wa kuondoa magugu na kufanya shamba kuwa safi na malisho
kustawi vizuri kwa wakati na linakuwa na rutuba ya kutosha,” alisema Rottcher
“Kulisha chakula cha kutosha na cha
aina tofauti husaidia mnyama kupata virutubisho vingi vinavyosaidia
kujenga afya ya mifugo,” Aliongeza Rottcher
Aidha, aliwashauri Wakurugenzi na
Mameneja wa mashamba ya Serikali kutoa mifugo kwenda kujitafutia chakula na sio
kuwaletea katika maboma yao kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia mifugo kupata
kile wanachotaka na sio kuwapimia chakula jambo ambalo litawezesha kupata
mifugo iliyo bora yenye nyama nyingi na maziwa ya kutosha yenye viwango.
Akieleza kuhusu ziara yao katika
Shamba hilo, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani Dkt. Kejeri Gillah alisema
lengo ni kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuboresha kosaafu na utunzaji
wa mifugo, ustawishaji wa malisho bora kwa mifugo ya aina mbalimbali na namna
ya uhifadhi wa malisho kwa matumizi ya kipindi cha kiangazi.
“Ni mategemeo yetu kwamba safari hii
itakuwa ya mafanikio makubwa sana kwetu na tutaweza kuboresha mifugo yetu na
kustawisha malisho ya mifugo kama tutafuata yale yote tutakayoelekezawa”
alisema Dkt. Gillah
Ziara hiyo iliratibiwa na Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Ugani, ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za
Ugani, Dkt. Kejeri Gillah, wengine walishiriki katika ziara hiyo ni Mameneja
kutoka Shamba la kitulo, Sao hill, Langwira, Vikuge, Mkurugenzi wa Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Uyole na meneja wa Ranchi ya Kalambo.
Afisa Utafiti Mifugo Mkuu
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Felista Kimario akitoa neno la shukrani
kwa Mtendaji Mkuu wa shamba la Ndoto, Bw. Hartmut Rottcher (hayupo pichani) kwa
kutumia muda wake kuwatembeza kwenye shamba hilo na kuwaelimisha mambo
mbalimbali katika upandaji wa malisho, namna ya kutunza na kulisha Mifugo.
(27.11.2020)
Mtendaji Mkuu wa shamba la
Ndoto, Bw. Hartmut Rottcher (wa pili kutoka kulia) akiwatembeza watumishi wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliofika shambani hapo kujionea na kujifunza namna ya ustawishaji wa
malisho, uboreshaji wa kosaafu na utunzaji Mifugo. (27.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Uyole Mbeya, Dkt. Edwin Peter Chang'a (katikati)
akiuliza swali kwa Mtendaji Mkuu wa shamba la Miombo, Bw. Rex Fey (wa pili
kushoto) wakati wa safari yao ya Mafunzo Mkoani Iringa. (27.11.2020)
Mtendaji Mkuu wa shamba la
Ndoto mkoani Iringa, Bw. Hartmut Rottcher akiwaeleza watumishi wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi aina ya nyasi za malisho zilizopo shambani hapo na namna
anavyofanya kilimo cha malisho ya Mifugo. (27.11.2020)
Watumishi kutoka katika
mashamba mbalimbali ya Mifugo yaliyopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa shamba la Miombo, Bw. Rey Fey (kushoto) wakati
akizungumzia kuhusu mbegu, malisho na namna bora ya kulisha Mifugo kwenye
shamba la Ndoto lililopo mkoani Iringa. (27.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi Ugani Mifugo
kutoka WMUV, Dkt. Kejeri Gillah akieleza lengo la safari yao ya Mafunzo wakati
walipotembelea shamba la Ndoto mkoani Iringa, kuwa ni kubadilishana uzoefu
katika uboreshaji wa kosaafu, utunzaji Mifugo, uhifadhi bora wa malisho,
Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya madawa. (27.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi Ugani Mifugo
kutoka WMUV, Dkt. Kejeri Gillah akieleza lengo la safari yao ya Mafunzo wakati
walipotembelea shamba la Ndoto mkoani Iringa, kuwa ni kubadilishana uzoefu
katika uboreshaji wa kosaafu, utunzaji Mifugo, uhifadhi bora wa malisho,
Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya madawa. (27.11.2020)
SERIKALI YAJIPANGA KUIMARISHA SEKTA YA UVUVI NCHINI
Na Mbaraka Kambona, Singida.
Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ipo katika mchakato wa kukamilisha Mpango kabambe wa miaka 15
ijayo kuanzia 2021 utakaosimamia sekta ya Uvuvi na kutoa dira ya kulinda
rasilimali za uvuvi ili sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa na endelevu
katika pato la taifa.
Hilo limefahamika wakati
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifungua
Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Uvuvi wa kupitia, kujadili na kuidhinisha masuala
ya kipaumbele yanayopaswa kuingizwa katika Mpango huo Kabambe unaofanyika
Mkoani Singida Novemba 26-28, 2020.
Dkt. Tamatamah alisema kuwa
lengo la Serikali ni kuona sekta ya Uvuvi inaendelea kutoa mchango mkubwa
katika pato la taifa zaidi ya ilivyosasa na ndio maana inaanda Mpango huo ili
usimamizi wa rasilimali za uvuvi uwe imara.
“Ni mategemeo yetu kuwa
mpango huu utatoa hamasa kwa sekta ya uvuvi katika kulinda usalama wa chakula
kuanzia ngazi ya kaya na taifa, vilevile tunatarajia utuingize katika uchumi wa
viwanda na uchumi wa bluu,” alisema Dkt.Tamatamah
Alisema kuwa pamoja na juhudu
za Wizara za kusimamia maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini, Sekta hiyo imeendele
kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa ujumla zimekuwa zikiathiri
ukuaji na uendelevu wa sekta hiyo.
Aliendelea kueleza kuwa ili
kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imekuwa ikitekeleza mipango, mikakati na
programu mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya uvuvi nchini, miongoni mwa
mipango hiyo ni Mpango huo Kabambe wa Uvuvi unaotarajiwa kuanza kutumika mwaka
2021.
Mratibu wa Masuala ya Uvuvi
kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ambao wanafadhili maandalizi
ya mpango huo, Dkt. Oliver Mkumbo alisema shirika hilo limeamua kufadhili
mpango huo ikiwa ni sehemu ya malengo yao ya kuhakikisha dunia inaondokana na
njaa, umasikini na kuimarisha usalama wa chakula ili ifikapo mwaka 2030
pasiwepo na mtu atakayekuwa na njaa.
Aidha, wadau wa Sekta ya
Uvuvi hawakusita kuonesha matumaini yao na mpango huo huku wakisema kuwa
ukikamilika utajibu changamoto nyingi ambazo zimeendelea kukabili sekta hiyo.
Kiongozi wa Wavuvi Mkoani
Kigoma, Francis John alisema kuwa mpango huo ambao utasimamia rasilimali za
uvuvi utawasaidia kuimarisha biashara yao ya dagaa kutoka ziwa Tanganyika kwani
mpango huo utawahakikishia uwepo wa dagaa wengi ambapo wataweza kuwa na mzigo
wa uhakika wa kusafirisha kwenda kuuza dagaa wao katika nchi za Marekani,
Astralia, Kanada, Uingereza na Denmark.
Naye, Raphael John, mdau wa
sekta hiyo ya Uvuvi alisema kuwa moja ya
mambo yatayokwenda kuimarishwa kupitia mpango huo ni ufugaji na ukuzaji wa
viumbe maji jambo ambalo anasema litasaidia kupunguza utegemezi wa kupata mazao
ya uvuvi kutoka maji ya asili pekee.
“Katika nchi nyingi
zilizoendelea, ufugaji na ukuzaji wa viumbe maji umepewa kipaumbele sana, ni
muhimu kuimarisha eneo hilo ili tusitegemee tu uvuvi wa mazao ya samaki katika
maji ya asili, ni lazima tuanze sasa kabla rasilimali za asili katika bahari,
mito na maziwa hazijaisha,” alisema John
Mpaka sasa sekta ya uvuvi
inachangia asilimia 1.7 katika pato la Taifa huku ikielezwa kuwa sekta hiyo
inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wananchi takriban 202,000 na wananchi wengine
wasiopungua Milioni 4.5 wamaendelea kutegemea kupata kipato chao kupitia sekta
hiyo.
Shirika la Chakula na Kilimo
Duniani (FAO) limetoa Dola za Kimarekani 195,000 kwa ajili ya kufanya mapitio
na kuandaa Mpango huo Kabambe wa sekta ya uvuvi ili sekta hiyo iweze kusimamiwa
vizuri na kuendelea kuleta maendeleo yenye tija nchini.
Uandaaji wa mpango huo ni sehemu ya mipango mingi ambayo serikali imekusudia kuitekeleza, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 13, 2020 jijini Dodoma, Mhe. Rais, Dkt. John Joseph Magufuli alieleza mipango kadhaa ya kuboresha sekta ya uvuvi ikiwemo ununuzi wa meli nane (8), ujenzi wa Bandari kubwa ya uvuvi itakayotoa ajira elfu thelathini (30,000).
PROF. OLE GABRIEL AWAFUNDA WASOMI HOMBOLO
Na Mbaraka Kambona,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amewaeleza wanafunzi wa Chuo cha
Serikali za Mitaa- Hombolo kuwa wao ni Viongozi watarajiwa hivyo wanawajibu wa
kuhakikisha watakapokuwa viongozi wanakidhi matarajio ya wale watakaokuja
kuwaongoza.
Prof. Gabriel aliyasema hayo
wakati akiwasilisha mada iliyohusu nafasi ya viongozi wa kuchaguliwa katika
kuleta maendeleo kwa jamii anayoiongoza kwenye hafla ya kuwatunuku zawadi
wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao na wafanyakazi bora wa chuo cha
Hombolo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma Novemba 25, 2020.
Alisema kuwa katika kipindi
hiki ambacho nchi ya Tanzania imeingia katika uchumi wa kati viongozi
wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wanakidhi matarajio ya Watanzania.
Prof. Gabriel aliongeza kuwa
nchi nyingi na taasisi zimekuwa zikikwama kufikia malengo tarajiwa kwa sababu
ya kukosa usimamizi mzuri.
“Kuwa na rasilimali ni jambo
moja, lakini kusimamia rasilimali hizo ni jambo la muhimu zaidi, taasisi nyingi
zimekwama kwa kushindwa kusimamia rasilimali zake ikiwemo rasilimali watu,
rasilimali fedha na rasilimali miundombinu,” alisema Prof. Gabriel
Kwa mantiki hiyo aliupongeza
Uongozi wa Chuo cha Hombolo kwa kusimamia agenda ya uongozi huku akisema kuwa
elimu hiyo wanayoitoa kwa wanafunzi wa chuo hicho itawasaidia wanafunzi hapo
mbeleni watakapokuwa viongozi.
Aliendelea kusema kuwa
kiongozi yeyote wa kuchaguliwa au kuteuliwa ili awe kiongozi bora ni muhimu
kuzingatia mambo matatu ambayo ni kufahamu hasa anaowaongoza wanamahitaji gani?
pia Kiongozi atambue kuwa hatakumbukwa kwa cheo chake bali kwa mchango wake kwa
jamii ile anayoiongoza na tatu, awe mtu anayewashirikisha wale anaowaongoza
katika kutatua changamoto zao.
“Washirikishe wale
unaowaongoza na ndipo utakapoweza kutatua changamoto, kiongozi mzuri ni yule
anayeziona changamoto na kuzibadilisha kuwa fursa, na kwa kufanya hivyo ndipo
utaweza kukidhi matarajio ya wale unaowaongoza,”alisisitiza Prof. Gabriel
Katika hafla hiyo ya kumi na
mbili (12) ya chuo hicho, Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa Mtoa mada maalum
na aliwasilisha mada hiyo ya nafasi ya viongozi wa kuchaguliwa na wakuteuliwa
katika kuleta maendeleo kwa jamii ili kuwakumbusha wajibu wao mkubwa kwa jamii.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), akifurahia jambo
alipokuwa akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli
(kushoto) walipokutana kwenye Hafla ya
Kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa-
Hombolo waliofanya vizuri katika masomo.
Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa Mtoa mada maalum katika hafla hiyo
iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)
Sehemu ya Wanafunzi na
Wafanyakazi wa Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo waliohudhuria hafla ya
kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo
iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasalimia Wanafunzi na
Wafanyakazi wa Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo (hawapo pichani) alipokuwa
akitambulishwa katika hafla ya kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi
waliofanya vizuri katika masomo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma.
(25.11.2020)
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada katika hafla ya
kutunukiwa zawadi Wafanyakazi na Wanafunzi waliofanya vizuri wa Chuo cha
Serikali za Mitaa-Hombolo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma.
(25.11.2020)
BARAZA LA VETERINARI LAKIFUNGIA KITUO CHA AFYA SENDEU
Baraza la Veterinari Tanzania limekifungia kituo cha huduma ya afya ya wanyama cha Sendeu kilichopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha kwa kubainika kutokuwa na wataalam waliosajiliwa na Baraza hilo.
Baraza limefikia hatua hiyo
mkoani humo Novemba 22, 2020 kufuatia ukaguzi unaoendelea kufanywa katika mikoa
mbalimbali nchini na wakaguzi wa baraza hilo ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya
kila siku.
Msajili wa Baraza Veterinari
Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli alieleza kuhusu uamuzi huo wa baraza ofisini
kwake, jijini Dodoma Novemba 23, 2020.
Dkt. Masuruli alisema kuwa
uamuzi huo wa baraza umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa kituo hicho cha afya
ya wanyama kinaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu.
Aliongeza kuwa wakaguzi wa
baraza walipoenda kufanya ukaguzi katika kituo hicho walibaini mapungufu hayo
ambayo kimsingi ni kinyume cha taratibu na ni hatari kwa afya ya wanyama.
Aidha, Dkt. Masuruli aliwahimiza wamiliki wote
wa vituo vya afya ya mifugo kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinasimamiwa
kikamilifu na huduma zinazotolewa na wataalam wa mifugo waliosajiliwa na baraza
la veterinari Tanzania.
Dkt. Masuruli amevisisitiza
vituo vingine vyote nchini kuzingatia taratibu zote za kutoa huduma, na baraza
halitasita kuchukua hatua kwa vituo vyote vitakavyoshindwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za utoaji huduma ya afya ya wanyama.
Awali msajili wa Baraza hilo
alisema walifanya ukaguzi kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga, Simiyu na Ruvuma na
kubaini changamoto za ukiukwaji wa maadili ya utoaji huduma ya afya ya wanyama
na kupelekea kulipishwa faini na
wengine kufungiwa kutoa huduma ya afya ya wanyama.
WADAU WA UVUVI WAKUTANA KUPITIA MPANGO KAZI UVUVI MDOGO
Na Mbaraka Kambona,
Wadau wa Sekta ya Uvuvi kutoka maeneo mbalimbali wamekutana kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu nchini.
Akiongea wakati akifungua kikao kazi cha kupitia mpango huo wa kitaifa kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 21, 2020, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi alisema sekta ya uvuvi inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wavuvi wadogo wapatao 202,053 na zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanategemea shughuli zinazohusiana na uvuvi ikiwemo uchakataji na biashara ya samaki na mazao mengine.
Aliongeza kuwa pamoja na hali hiyo bado wananchi wengi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi ni masikini huku akisema kuwa hali hiyo haikubaliki na ni kinyume na maelekezo ya sera na miongozo mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ya nchi yetu ikiwemo Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015.
Bulayi aliendelea kueleza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kutatua changamoto zinazowakabili wavuvi ikiwemo uandaaji wa mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu.
Alisema mwongozo huo umeibua na kutoa njia ambazo zikitumika kikamilifu hali ya kiuchumi na kijamii ya wavuvi wadogo itaboreka kwa kiasi kikubwa huku rasilimali za uvuvi zikiendelea kuvunwa kwa njia endelevu.
“Usimamizi thabiti wa mwongozo huu unaweza kupelekea kuongezeka kwa ajira, kipato, chakula na lishe na hivyo wavuvi wengi kujikwamua katika umasikini uliopitiliza,”alisema Bulayi
“Nichukue fursa hii kulishukuru sana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari na kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu katika muktadha wa chakula na kuondoa umasikini,” aliongez Bulayi
Aidha, alisema pamoja na mwongozo huo kuwa umepangiliwa vizuri, kama utekelezaji wake hautasimamiwa ipasavyo, hautaweza kutoa tija inayotarajiwa na kwa kutambua hilo Wizara iliunda Kikosi Kazi cha Kitaifa mwaka 2018 ili kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Oliver Mkumbo alisema umuhimu wa mpango kazi kwa nchi ya Tanzania uko wazi ukizingatia sekta ya uvuvi inategemewa na watu wengi kwa shughuli mbalimbali za kujipatia kipato na lishe.
“Tunatambua juhudu za Serikali, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazotekeleza mpango huu, tunaipongeza serikali na wadau kwa kuona umuhimu wa mpango huu na ni matumaini yangu utasaidia kuleta maendeleo kwa wavuvi na jamii kwa ujumla,” alisema Mkumbo
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kusimamia mazingira nchini (EMEDO), Elitrudith Lukanga aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa mpango huo na alitoa wito kwa mashirika mengine kuhakikisha wanashiriki vyema katika mchakato wa utekelezaji wa mpango huo.
“Sisi kama sehemu ya wadau wa utekelezaji wa mpango huu tutashiriki kikamilifu katika kuhamasisha wadau mbalimbali hususani Wanawake kuuelewa mpango huu ili uwe sehemu katika shughuli zao za kila siku,” alisema Lukanga.
Jumamosi, 21 Novemba 2020
MRADI WA SWIOFISH WASHIRIKISHA WANANCHI KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi Mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) umewezesha uboreshaji wa miundombinu ya taasisi za wizara hiyo katika kuhakikisha serikali kwa kushirikiana na wananchi inalinda rasilimali za uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.
Akizungumza na wahariri wa
vyombo mbalimbali vya habari nchini katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na
Uvuvi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafahamisha manufaa ya mradi wa
SWIOFish, Dkt Tamatamah amesema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia
umewanufaisha pia wavuvi wa Pwani ya Bahari ya hindi, wakulima wa Mwani,
wafugaji wa viumbe maji na wachakataji wa mazao ya uvuvi wakiwemo wanawake na
jamii inayozunguka maeneo hayo.
“Lengo kuu la mradi huu ni
kuimarisha usimamizi madhubuti wa uvuvi katika ngazi ya kijamii, kitaifa na
kimataifa na malengo mengine ni kujenga uwezo wa nchi katika kusimamia
rasilimali za uvuvi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika ulinzi wa
rasilimali za uvuvi wa Bahari kuu, kuinua uchumi wa jamii ya watu wa Pwani na
kuinua pato la taifa kutokana na rasilimali za uvuvi,” Amesema Dkt. Tamatamah.
Aidha, Dkt. Tamatamah amesema
tangu mradi huo uingie hapa nchini mwezi Juni mwaka 2015 ambapo unatarajia
kukamilika mwezi Septemba mwaka 2021 uvuvi haramu wa kutumia baruti na mabomu
umedhibitiwa kwa asilimia 100 kutokana na kuimarishwa kwa doria pamoja na
kuongezeka kwa uelewa wa jamii ya Pwani kuhusu madhara ya uvuvi haramu.
Pia, amesema usajili wa
vyombo vya uvuvi umeongezeka hadi kufikia asilimia 58 kutoka asilimia 25 ya
awali kabla ya mradi kutokana na usimamizi wa utekelezwaji wa sheria na kanuni
za uvuvi. Mradi umewezesha tafiti mbalimbali ambapo matokeo yake yametumika
kurekebisha baadhi ya kanuni za uvuvi ambazo zimesaidia kuongezeka kwa samaki
wanaovuliwa pamoja na kuongezeka kwa uvuvi wa karibu wa kutumia ndoano kwa
maeneo mengi.
“Mafanikio mengine ya Mradi
wa SWIOFish ni pamoja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na uvuvi hususan
kwenye halmashauri ambapo Halmashauri ya Pangani yameongezeka kutoka milioni 55
mwaka 2016/17 hadi kufikia Milioni 235 mwaka 2018/19,” Amebainisha Dkt.
Tamatamah.
Katika kikao hicho na
wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah ametumia muda huo kuelezea pia namna mradi wa
SWIOFish ulivyoimarisha Sekta ya Uvuvi kwa kufadhili mafunzo ya uvuvi endelevu
ambayo yamesaidia baadhi ya wavuvi kutekeleza kwa hiari usimamizi wa rasilimali
za bahari.
Ameongeza kuwa mradi
umeanzisha vikundi hamsini vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi
(BMU) katika Wilaya tano za mfano na kuimarisha utunzaji wa mazingira ya Pwani,
viwango vya dagaa pamoja na Mwani vimeandaliwa na kupitishwa na Shirika la
Viwango Tanzania (TBS).
Katibu mkuu huyo pia amesema
mradi umewezesha ujenzi wa maabara ya utafiti iliyoko Taasisi ya Utafiti wa
Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaaam, ujenzi wa nyumba tatu za
watumishi wa Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), kituo cha
Tanga Silikanti kilichopo Kigombe, wilayani Muheza, na ujenzi wa ofisi tano za
BMU katika Wilaya za Mkinga (Zingibari), Pangani (Kipumbwi), Chalinze
(Saadani), Bagamoyo (Dunda) na Lindi vijijini (Sudi).
Kwa upande wake Mratibu wa
mradi wa SWIOFish Tanzania Bara, Bw. Nichrous Mlalila amesema licha ya
mafanikio ya mradi changamoto mbalimbali zimekuwa zikijitokeza zikiwemo za
ugumu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za
BMU, kutokea kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu wa kutumia nyavu zisizofaa
kisheria na upatikanaji wa takwimu sahihi katika mifumo ya ukusanyaji taarifa.
Bw. Mlalila amesema hadi sasa
asilimia 65 ya shughuli za mradi zimetekelezwa na kukamilika, ambapo asilimia
nane (8) zipo katika utekelezaji kwa zaidi ya asilimia 75, asilimai 19 ya
shughuli za mradi zinaendelea kutekelezwa kati ya asilimia 25 hadi 75 ya
utekelezaji. Asilimia nne (4) zipo katika utekelezaji wa asilimia chini ya 25.
Ameongeza kuwa mradi unaonyesha
matokeo chanya na upo katika mwelekeo mzuri wa utekelezaji.
Akizungumza kwa niaba ya
wahariri wa vyombo vya habari waliohudhuria kikao hicho Kaimu Mhariri Mkuu wa
gazeti la Habari Leo Bw. Mgaya Kingoba ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Sekta ya Uvuvi kwa kuendelea kuwapatia taarifa mbalimbali na elimu juu ya sekta
hiyo ambazo zinawasaidia kutoa taarifa sahihi kwa umma.
Pia, amewaomba wahahriri
wenzake kuendelea kuiunga mkono wizara hiyo katika kuhakikisha inatoa taarifa
ambazo zitasaidia kulinda rasilimali za uvuvi pamoja na kupambana na uvuvi
haramu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mradi wa SWIOFish
unatekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi ya
Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi
Tanzania (FETA) na Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU)
katika maeneo ya Pwani ya Tanzania katika wilaya tano za mfano zikiwemo Mkinga,
Tanga Jiji, Pangani, Bagamoyo na Lindi Vijijini. Kwa upande wa Zanzibar, Mradi
unatekelezwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi pamoja na Mamlaka
ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA).
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na Wahariri wa Vyombo
mbalimbali vya habari, baada ya kufungua kikao hicho chenye lengo la kuelezea
mafanikio ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini
Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) katika ofisi ndogo za wizara hiyo
jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)
Mratibu wa Mradi wa Usimamizi
Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi
(SWIOFish) Tanzania Bara, Bw. Nichrous Mlalila akiwaelezea wahariri wa vyombo
vya habari (hawapo pichani) waliohudhuria kikao hicho kilichokuwa na lengo la
kuwaelezea wahariri hao mafanikio ya mradi wa SWIOfish. Kikao hicho kimefanyika
katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam.
(20.11.2020)
Wahariri wa vyombo mbalimbali
vya habari hapa nchini wakipata maelezo na kushuhudia namna serikali
inavyofuatilia vyombo vya majini vinavyofanya shughuli za uvuvi maeneo ya
bahari kuu, wakati wa kikao cha Sekta ya Uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari
kilichokuwa na lengo la kuwafahamisha mafanikio ya Mradi wa (SWIOFish). Kikao hicho
kimefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es
Salaam. (20.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha
ya pamoja na wahariri wa vyombo vya habari nchini, na baadhi ya maafisa kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya mradi wa SWIOFish, baada ya kufungua kikao
cha Sekta ya Uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari kuelezea mafanikio ya
mradio huo. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini
Dar es Salaam. (20.11.2020)
USHIRIKIANO WA BODI YA MAZIWA NA SEKTA BINAFSI KUONGEZA USINDIKAJI WA MAZIWA HAPA NCHINI
Bodi ya Maziwa yasisitiza ushirikiano na sekta binafsi katika kuongeza usindikaji wa maziwa nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili wa
Bodi ya Maziwa, Bw. Noely Byamungu wakati wa kikao kazi cha kubainisha maeneo
ya ushirikishwaji na Sekta Binafsi kilichofanyika jana (20.11.2020) jijini Dar
es Salaam.
Kikao kazi hicho kililenga
kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano 2020/21-2025/26 wa Bodi ya Maziwa na
kubainisha namna ya bora ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utekelezaji
wa majukumu ya Bodi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakurugenzi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Makampuni ya Wasindikaji
Maziwa ya UHT nchini kutoka kampuni ya Asas Dairies, Tanga Fresh, Milkcom na
Azam Dairies, Wabia wa maendeleo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB) na Mradi wa Wasindikaji wa Maziwa Tanzania (TMPP).
Bw. Byamungu alisema kuwa
lengo la Bodi ya Maziwa ni kuwezesha viwanda kuongeza uwezo wa kusindika maziwa
ambao kwa sasa usindikaji wa maziwa katika viwanda hivyo ni asilimia 23.52.
Aidha, Msajili amesema kuwa
Bodi ya Maziwa ipo tayari kuunga mkono jitihada za wadau wa Tasnia ya Maziwa
kufikia malengo yao ya kuzalisha maziwa kwa kiwango kilichosimikwa.
Bw. Byamungu alisema kuwa
kikao hicho kitaleta mtazamo wa muda mrefu wa Tasnia ya maziwa katika
usindikaji na kutoa ramani ya kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wadau,
mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa sekta binafsi, wabia wa maendeleo na
wadau wengine kwenye sekta.
"Bodi ya Maziwa iko
tayari na ina nia njema ya kufanya kazi pamoja nanyi kufikia malengo ya kuwa sekta
endelevu katika uzalishaji, usindikaji na masoko ya maziwa na bidhaa zake
nchini" Alisema Bw. Byamungu.
Nae Mkurugenzi wa Mradi wa
Wasindikaji Tanzania, Bw. Mark Tsoxo amesema wapo tayari kuisaidia Bodi ya
Maziwa kutekeleza majukumu yake ya kuongeza usindikaji wa maziwa nchini ili
kuimarisha mnyororo mzima wa thamani. Pia ameiomba Bodi ya Maziwa kuendelea
kushirikiana na Sekta Binafsi kwa Ukaribu ili kufikia azma iyo.
Tasnia ya Maziwa ina mchango
mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umaskini.
Washiriki wa kikao cha
"Stakeholder Engagement Towards Sustainable Dairy Industry in
Tanzania" wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kikao kilichofanyika jijini
Dar es Salaam. (20.11.2020)
Kaimu Msajili wa Bodi ya
Maziwa, Bw. Noel Byamungu (wa kwanza kushoto) akisikiliza kwa makini mada
zinazowasilishwa na mdau (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha kuimarisha
mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es
Salaam. Kulia ni mwakilishi kutoka Azam Dairies, Bw. Yunus Ibrahim.
(20.11.2020)
Mhandisi kutoka Wizara ya
Viwanda na Biashara, Bw. Emmanuel Zakayo (kushoto) akifuatiwa na Mchumi Mkuu
kutoka Wizara ya Viwanda, Bi. Genoveva Kilabuko na Mchumi kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Bw. Francis Makusaro wakati wa kikao kazi cha kuimarisha
mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es
Salaam. (20.11.2020)
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe (WMUV), Bw. Gabriel Bura akisikiliza kwa makini mada zinazowasilishwa wakati wa kikao kazi cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)
Mkurugenzi Mtendaji wa
Kiwanda cha Tanga Fresh, Bw. Innocent Mushi akisikiliza mada zinazowasilishwa
wakati wa kikao cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali
kilichofanyika jijini Dar. Es Salaam. (20.11.2020)
Baadhi ya Wasindikaji wa
Maziwa wakiwa kwenye kikao cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na
Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi
kutoka Milkcom Dairies, Bw. Abubakar Faraji, akifuatiwa na Abdul Ally kutoka ASAS
Dairies na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi mtendaji kutoka Tangafresh, Innocent
Mushi. (20.11.2020)