Serikali imesema inataka kuona uanzishwaji wa
viwanda vidogo vidogo vya wafugaji na wavuvi kupitia mikopo inayotolewa na
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuyaongezea thamani mazao
yanayotokana na sekta za mifugo na uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega amezungumza hayo (30.05.2020) katika Kijiji cha Kanyala
kilichopo Halmashauri ya Buchosa iliyopo Wilaya Sengerema Mkoani Mwanza, wakati
wa kukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 uliotolewa na TADB kwa Chama cha
Ushirika cha Zilagula ambacho pia kimepata mkopo wa Shilingi Milioni Tano
kutoka katika mfuko wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Mhe. Ulega amesema licha ya vyama
vingine vya Kasalazi na Soswa ambavyo kila kimoja kimepata pia mkopo wa
halmashauri wa Shilingi Milioni Tano, ili wafugaji na wavuvi waweze kunufaika
na mikopo kupitia ushirika wao, wizara itakuwa msimamizi kwa vyama
vitakavyokidhi sifa za kupata mikopo kutoka TADB.
“Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaenda
kuwa msimamizi namba moja wa vyama vya ushirika tena kwa barua hivyo niwatakeni
uongozi wa mkoa, halmashauri na ushirika wekeni taarifa zenu vizuri. Tunataka
viwanda vidogo vidogo vya wafugaji na wavuvi vikiwemo vya kukausha dagaa,
minofu ya samaki na kutengeneza kayabo nzuri ili mpeleke bidhaa hizo kwenye
masoko ya ndani na nje ya nchi.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega amevitaka vyama
hivyo vitatu vilivyopata mikopo waitunze mikopo hiyo kwa kuifanyia kazi na
hatimaye kuirejesha, kikiwemo Chama cha Zilagula kilichopata mkopo kutoka TADB,
kwa kuwa fedha zilizotolewa na benki hiyo zinamilikiwa na watanzania kwa
asilimia mia moja ili watanzania wengine pia waweze kunuifaika na mikopo
hiyo na kutoa rai kwa wavuvi kuendelea kujiunga katika vyama vya ushirika
wakati akikabidhi hati ya kuandikishwa kwa vyama vya Sangara-Nyakaliro na
Gembare vilivyopo Halmashauri ya Buchosa.
Amewataka pia watendaji wa serikali
kutoa elimu kwa vyama vya ushirika namna ya kuitumia vyema mikopo wanayopata
ili waweze kuirejesha kwa wakati pamoja na kuwaongoza ili waweze kupata mikopo
mikubwa zaidi kwa kuwa utoaji mikopo kwa vyama vya ushirika vya wafugaji na
wavuvi ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli
kwa kutaka kuona wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo hapa nchini.
“Watendaji wakati mwingine vyama vya
ushirika havikosei kufikia hatua mbaya ya kukosa mikopo ni muhimu elimu itolewe
na watendaji kwa wafugaji na wavuvi msiwaache hawa watu wa ushirika waliopatiwa
mikopo kwa kuwapatia elimu na kuwaongoza hatua kwa hatua ili waweze kulipa
marejesho ya mikopo waliyopatiwa.” Amefafanua Mhe. Ulega
Vilevile, Naibu Waziri Ulega
amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kujiepusha na ubadhilifu wa fedha za
mikopo hiyo kutoka TADB, huku akitoa rai kwa wavuvi kuwa na uchumi endelevu na
hatimaye kuwa walinzi wa rasilimali za uvuvi kupitia vyama vyao vya ushirika
kwa kuwa azma ya serikali ni kuona Tanzania inaongoza kwa kusafirisha minofu ya
samaki kwenda nje ya nchi na mchango wa samaki katika pato la taifa unaongezeka
kutoka Asilimia 1.7 hadi Mbili ya sasa na kufikia Asilimia Tano na kuendelea.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine ameishukuru
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka mikakati mizuri na benki hiyo iliyowezesha
kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanakuwa na sifa za
kupatiwa mikopo ili kujiendeleza katika sekta hizo.
“Tuliomba kwanza vyama hivi vikae
katika ushirika kwa sababu tuliamini ule umoja wao utatupatia njia kuhakiksha
mikopo inalipwa kwa kuwaweka katika mfumo ulio rahisi, wizara pia iliweka
mazingira ya kubadilisha mitumbwi kuwa na namba na kufahamika ili benki iweze
kuwa na taarifa sahihi ya mitumbwi ya wahusika wanaopatiwa mikopo pamoja na
kuweka mazingira ya wavuvi kuwa na mifumo rasmi ya kuweka na kutoa pesa ili
benki iweze kujua historia na kutoa mikopo kulingana na historia ya waombaji.”
Amebainisha Bw. Justine
Bw. Justine ameongeza kuwa TADB
inatoa mikopo hiyo na nia yao ni kuona wafugaji na wavuvi wengine wengi
wananufaika na mikopo hiyo na kuwataka kufanya biashara zao kwa kuweka
kumbukumbu zao vizuri ili wanufaika waweze kufikia hatua ya kuwa na viwanda
vidogo vidogo.
Aidha, amesisitiza kwa vyama vya
ushirika vilivyopata mkopo kutoka TADB kuhakikisha vinalipa mikopo hiyo kwa
wakati ili watanzania wengine wenye uhitaji wa kupata mikopo hiyo waweze kupata
na kukuza biashara zao.
Kuhusu Dawati La Sekta Binafsi
lililo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambalo limekuwa likifanya kazi kubwa
katika kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanaunganishwa na taasisi mbalimbali za
kifedha, Mratibu wa dawati hilo Bw. Steven Michael amesema kazi yao kubwa ni
kuhakikisha matokeo chanya yanaonekana likiwemo tukio la Chama cha Ushirika cha
Zilagula kupatiwa mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 kutoka TADB.
Bw. Michael amesema wamefanya kazi
kubwa kuhakikisha vyama vya ushirika wanaviunganisha na taasisi za kifedha
pamoja na halmashauri mbalimbali nchini na kufuatilia mara kwa mara kwa kuwa
wao wanafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wadau wa mifugo na uvuvi na taasisi
hizo kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha
Ushirika Zilagula Bw. Joram Yuda amesema wanaishukuru serikali kwa kuwa wavuvi
wameanza kuaminika na taasisi za kifedha kwa kuwapatiwa mikopo ili kujiendeleza
katika sekta hiyo, huku Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Gembare Bw. Hassan
Muhenga ameishukuru pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TADB kwa
kuhakikisha wanasimamia maono ya Rais Dkt. John Magufuli ya wkupatiwa mikopo.
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akisalimiana na wananchi mara baada ya kuwasili
katika kijiji cha Kanyala kilichopo Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema
Mkoani Mwanza kwa ajili ya kutoa mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo
(TADB) na Halmashauri ya Buchosa kwa vikundi vya ushirika vya wavuvi.
(30.05.2020)
|
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah
Ulega akizungumza na baadhi ya wananchi na vikundi vya ushirika wa wavuvi
wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mikopo kwa vikundi hivyo kutoka TADB na
Halmashauri ya Buchosa na kutaka mikopo hiyo iwe chachu kwa wavuvi kuanzisha
viwanda vidogo vidogo. (30.05.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah
Ulega akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TADB Bw. Japhet Justine (aliyevaa miwani)
kwa namna benki yake ilivyowezesha kutoka mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 kwa
Chama cha Ushirika Zilagula kilichopo Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya
Sengerema Mkoani Mwanza. (30 05.2020
Walioshika mfano wa hundi: Kutoka kushoto,
Mkurugenzi Mkuu wa TADB Bw. Japhet Justine, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Zilagula Bw. Joram Yuda
na Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi Bw. Steven Michael .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni