Serikali ya awamu ya tano katika
kipindi cha awamu ya kwanza imeweka mikakati mizuri na kuthubutu kuhakikisha
wavuvi wanaanza kuaminika na kukopeshwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB).
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega amezungumza hayo katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, wakati
akikabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 200 kutoka TADB kwa Chama cha Ushirika wa
Wavuvi Bukasiga na kufafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Magufuli ameweka mazingira ya kufanya wavuvi waweze kuaminika na taasisi
za kifedha na kupewa mikopo ili kujiimarisha katika shughuli zao.
“Hii benki tangu ianze ina miaka
mitano sasa na katika miaka mitano ya Dkt. John Magufuli imewakopesha
watanzania katika nyanja za kilimo, mifugo na uvuvi zaidi ya Shilingi Bilioni
170 na tangu uhai wa taifa hili wavuvi wameanza kuaminika na kukopeshwa pesa.”
amesema Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa wavuvi walikuwa
wanaonekana ni watu wa kuhamahama lakini kwa uthubutu, uzalendo na utayari
wavuvi wanaanza kuaminika na kuhamasishwa kujiunga katika vikundi vya ushirika
na kupatiwa mikopo ya masharti nafuu ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, ibara ya 27 na msimamo wa Rais
Dkt. John Magufuli.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine akizungumza katika hafla
hiyo fupi ya kukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 200 kwa Chama cha Ushirika wa
Wavuvi Bukasiga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha barafu, amesema wameweza
kutekeleza upatikanaji wa mkopo huo baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka
mikakati ya kuhakikisha inatekeleza uvuvi uwe wa kisasa utakaoonesha fursa
zaidi.
Akitoa neno la shukran kwa niaba ya
wanachama wa kikundi cha Bukasiga makamu mwenyekiti wa chama hicho Bw. Jumbula
Lugola amesema wanashukuru kwa mkopo huo kwa kuwa shughuli zao za uvuvi
zitabadilika na kufanyika kisasa zaidi kwa kuwa CCM imeweka mkakati mzuri ili
kuhakikisha wavuvi wanaufaika kupitia mikopo.
Ameongeza kuwa kwa juhudi za Rais
Magufuli hatimaye wameweza kupatiwa mkopo na TADB wa Shilingi Milioni 200 na
kumuahidi Rais Magufuli kuwa mkopo waliopatiwa watahakikisha wanautumia vyema
ili uwanufauishe pia watanzania wengine.
Picha ya pamoja: Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyevaa koti jeusi) akiwa na
baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwemo Mratibu wa Dawati la
Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo Bw. Steven Michael (wa tatu kutoka
kushoto) ambaye ameongoza dawati lake kufanikisha mikopo ya wavuvi kutoka TADB.
(31.05.2020)
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni