Serikali imesema itaendelea
kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha inaboresha afya za mifugo
na upatikanaji wa madawa kwa wakati ili wafugaji waweze kunufaika na mifugo
yao.
Akizungumza mara baada ya
kukutana na Mkurugenzi wa Taasisi ya ZOETIS A.L.P.H.A katika Bara la Afrika
Dkt. Gabriel Varga ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma jana (Jumatatu
30.09.2019)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ili kufuga kisasa ni
muhimu kwa wafugaji kushirikishwa na wataalamu katika kutambua magonjwa ya
mifugo yao na kupatiwa elimu ya namna ya kuwahudumia mifugo.
Ameongeza kuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imejipanga vyema katika katika kutekeleza majukumu yake kwa
vitendo ili kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika sekta ya mifugo
nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiwa
katika mazungumzo na Dkt. Varga amesema taasisi hiyo ambayo katika bara la
Afrika inafanya kazi na taasisi ya Bill and Melinda Gates (BMGF), malengo yao
yanafanana na mikakati ya wizara katika kuhudumia ukuzaji viumbe kwenye maji
hivyo wizara inatarajia katika kipindi cha miaka miwili au mitatu itafanya kazi
na taasisi hiyo ya ZOETIS A.L.P.H.A. katika sekta ya uvuvi.
Dkt. Tamatamah amefafanua
kuwa ufugaji samaki kwa sasa hapa nchini unawekewa kipaumbele katika kuendeleza
na kuongeza uzalishaji wa samaki kwa kuwa mahitaji ya ulaji wa samaki
yameongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya ongezeko la idadi ya
watu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi
ya ZOETIS A.L.P.H.A katika Bara la Afrika Dkt. Gabriel Varga amewaambia makatibu
wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel anayeshughulikia
Mifugo na Dkt. Rashid Tamatamah anayeshughulikia Uvuvi, kuwa taasisi yake
inatarajia kuanzisha maabara hivi karibuni katika mikoa ya Iringa, Dar es
Salaam, Mwanza na Morogoro ili kuboresha afya ya wanyama.
Aidha. Dkt. Varga
amefafanua kuwa taasisi hiyo ambayo kwa sasa inahudumia nchi zaidi ya 100 kote ulimwenguni
imekuwa ikiwasaidia wafugaji wa bara la Afrika kwa kuwapatia elimu ya huduma ya
wanyama ili waweze kufuga kwa tija.
Mazungumzo hayo
yamehudhuiriwa pia na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Dkt. Hezron Nonga, Mkurugenzi
wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Dkt. Nazael Madala na Msajili wa Baraza la
Veterinari Tanzania Dkt. Bedan Masuruli wote kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni