Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imeshtukia kusuasua kwa uendeshaji wa kiwanda cha Tanga Fresh
hali iliyolazimu kuundwa tume kufanya uchunguzi wa namna kiwanda kinavyofanya
kazi ikiwemo kuchunguza mtambo unaotumika kusindika maziwa ya muda mrefu ambao
unadaiwa umekuwa ukiongeza gharama ya uendeshaji wa kiwanda hicho.
Akizungumza jana
(21.10.2019) katika kiwanda cha Tanga Fresh mjini Tanga, kwenye kikao kilichohusisha
menejimenti ya kiwanda pamoja na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji
wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) kinachomiliki asilimia 43 ya kiwanda
hicho.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefafanua kuwa serikali itahakikisha inachukua hatua
kunusuru kiwanda kufuatia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Magufuli alipotembelea kiwanda hicho mwaka 2017 na kuahidiwa na
menejimenti kusindika maziwa lita laki moja kwa siku ambapo katika ziara hiyo
Rais Magufuli aliwasaidia kupata hati iliyokuwa imekwama kwa miaka mingi,
kuondoa changamoto ya wanahisa juu ya hisa zao Tume ya Ushindani (FCC) hali iliyopelekea
kiwanda kuanza kujitanua na kuongeza uzalishaji wa maziwa ya muda mrefu (UHT)
ingawa kiwanda kiliamua kuchukua mkopo Benki ya Biashara (NMB), unaoonekana
kuwalemea na kutofanya vizuri sawa na ahadi kwa Rais Magufuli.
“Kwanza serikali imebaini
manunuzi ya mtambo wa kusindika maziwa ya muda mrefu kuwa ni mtambo uliyokwishatumika
na umenunuliwa kwa zaidi ya Shilingi Bilioni Sita, pia riba ya mkopo kuwa ni
kubwa na kuwa mzigo, hivyo nimeagiza iundwe tume ambayo tayari Mkuu wa Mkoa wa
Tanga ameiunda kuanzia leo kufanya uchunguzi wa mtambo ulionunuliwa ikiwemo
fedha ya kununulia mtambo huo na utaratibu uliotumika kununulia mtambo.”
Amesema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega ameitaka
bodi ya wakurugenzi wa kiwanda pamoja na wamiliki wakae pamoja na Benki ya
Kilimo (TADB) kuitaka benki hiyo kununua deni hilo ili kutoa nafuu kwa kiwanda
na kuondoa mzigo kwa wafugaji na kuinua kipato chao.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigella amesema tayari timu ya wataalamu wakiwemo
kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO) imeshaundwa ili
kubaini hali ya mtambo wa kusindika maziwa.
Bw. Shigella amefafanua kuwa
serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukihujumu Kiwanda cha Tanga
Fresh ikiwemo kununua mtambo wa kusindika maziwa usio na tija kwa kiwanda
hicho.
Nao baadhi ya wanachama wa
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU)
wamepongeza hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na
uongozi wa Mkoa wa Tanga kutafuta suluhu ya namna ya kuboresha Kiwanda cha
Tanga Fresh ili kiweze kuongeza uzalishaji na kuwanufaisha wafugaji ambao
wamekuwa wakiuza maziwa katika kiwanda hicho pamoja na kutaka kiwanda hicho
kiongeze bei ya kununua maziwa kutoka kwa wafugaji hao ambao hawaridhiki na bei
ya Shilingi 700 kwa lita moja.
Kikao baina ya Wizara ya
Mifugo na Uvuvi chini ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega,
uongozi wa mkoa wa Tanga, menejimenti ya kiwanda cha Tanga Fresh, bodi na
wamiliki wa kiwanda kinatarajiwa kuendelea hii leo (22.10.2019) ili kutafuta
suluhu ya kunusuru kiwanda hicho baada ya kupata hasara kwa miaka mitatu
mfululizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni