Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amehamasisha wavuvi nchini kujiunga katika vyama vya
ushirika wa wavuvi ili waweze kunufaika kiuchumi kupitia taasisi mbalimbali za
kifedha.
Naibu Waziri Ulega amesema
hayo katika Kijiji cha Kanyala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani
Mwanza wakati akiwa katika ziara ya kutembelea Mikoa ya Kanda ya Ziwa kujionea
shughuli mbalimbali za sekta ya mifugo na uvuvi na kuhamasisha wadau wa sekta
ya uvuvi kujiunga na vyama vya ushirika wa wavuvi ili waweze kunufaika
kiuchumi.
“Wavuvi wengi dhamana ya
nyumba ni kikwazo kikubwa mnapohitaji mkopo kutoka katika mabenki lakini katika
vyama vya ushirika sharti hilo halipo, vyama vya ushirika ndiyo mdhamini wenu
na ukizingatia nimezindua Wavuvi Akuanti iliyoanzishwa na Benki ya Posta
Tanzania (TPB) tunapokuwa na vyama imara vya ushirika mtakuwa na nguvu na
kuweza kupata mikopo yenye masharti nafuu”. Alisema Mhe. Ulega
Aliongeza kuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati ya lazima kuanzishwa kwa vyama vya ushirika
vya wavuvi ili wadau wa sekta ya uvuvi waweze kusonga mbele kiuchumi na
kubainisha vyama hivyo ni lazima kuhusisha wachakataji, mafundi wa boti na
wavuvi na kwamba anataka biashara ya mazao ya samaki katika Ziwa Victoria
linalochangia asilimia 60 ya mapato ya samaki nchini kuongezeka na kuchangia
zaidi pato la taifa.
Naibu Waziri Ulega
alibainisha kuwa kukua kwa uchumi wa wadau wa sekta ya uvuvi nchini kutakuwa chachu
ya kuongezeka viwanda vya kuchakata samaki nchini huku akitaka wavuvi nchini
kuwa na uwezo wa kupata mitaji ya biashara ili waweze kufanya biashara zaidi
hususan katika ukanda wa Ziwa Victoria ambalo Tanzania inamiliki asilimia 51,
Uganda asilimia 43 na Kenya asilimia sita.
Kwa upande wake Mratibu wa
Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen
Michael alisema kazi kubwa ya dawati ni kuwaunganisha wafugaji na wavuvi na
kuhakikisha wanainuka katika uwekezaji na malengo makubwa ni kuhakikisha vyama
vya ushirika vya wavuvi vinapata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha.
Naye Afisa Ushirika wa
Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Bw. Martin Kimisha akisoma taarifa fupi ya uanzishwaji
wa vyama vya ushirika wa wavuvi, alisema hadi kufikia mwezi Novemba mwaka 2019 wanatarajia
kuwepo kwa vyama vitano ili waweze kunufaika ikiwa ni pamoja na kumudu
uchakataji wa zao la samaki na bidhaa zake na kuyafikia masoko ya ndani na nje
ya nchi.
Aidha Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Aballah Ulega akiwa mkoani Mwanza katika ziara yake ya kikazi
ya siku tatu alifika katika Wilaya ya Ukerewe na kuzungumza na wakazi wa kisiwa
cha Ukara ambapo aliwataka kulinda na kusimamia rasilimali za uvuvi nchini.
Mhe. Ulega alifafanua kuwa
pindi wananchi hao watakapolinda rasilimali hizo watakuwa katika fursa nzuri
zaidi kwa wao kunufaika na mazao ya samaki pamoja na kujiwezesha ili kujiunga
katika vyama vya ushirika wa wavuvi kwa ajili ya kupata mikopo na kuboresha
zaidi shughuli zao.
Aliongeza kuwa changamoto
mbalimali alizozibaini katika kisiwa hicho zitatatuliwa na kuutaka uongozi wa
Wilaya ya Ukerewe kuhakikisha unawakabidhi mashine za uvuvi watu wote ambao
mashine zao zilikamatwa lakini walishalipia faini walizotozwa kutokana na
makosa mbalimbali ya uvuvi katika Ziwa Victoria.
“Wale ambao walishalipia
lakini hawajapewa mashine zao baada ya kukamatwa mashine hizo kutokana na
makosa mbalimbali kwenye shughuli za uvuvi wakabidhiwe mashine zao.”
Alibainisha Mhe. Ulega
Akiwa katika kisiwa hicho
Mhe. Ulega aliwahamasisha pia wananchi hususan wanaohusika na shughuli za uvuvi
kujiunga katika vyama vya ushirika wa wavuvi ili waweze kupata mikopo na kukuza
shughuli zao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akibadilishana mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Bw. Carmel Maghembe mara baada ya kuhitimisha ziara yake wilayani humo. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni