Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na
wawekezaji kutoka Jamhuri ya Ireland wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya
maziwa hapa nchini na kuwataka kuangalia zaidi mnyororo wa thamani wa namna ya
kuyaongezea thamani maziwa ili kupanua zaidi soko la maziwa kutoka Tanzania
kwenda nchi za nje.
Akizungumza na wawekezaji
hao (Jumatatu 30.09.2019) kutoka shirika la Sustainable Food Systems Ireland
(SFSI) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Prof. Gabriel
amesema maziwa yatakapoongezewa thamani yataiwezesha Tanzania kuingia zaidi
katika masoko ya nje ya nchi yakiwemo ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya
Ushirikiano na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
“Waangalie pia zaidi
mnyororo wa thamani namna ya kuyaongezea maziwa thamani ili tuingie zaidi katika
solo la Afrika Mashariki, SADC na nje ya SADC. Lengo kubwa la wizara kwa wadau
kama hawa wakija kutuona inakuwa faraja kwa kuwa inagusa maisha ya mfugaji wa
kawaida, pale ambapo maziwa yatachakatwa na kuongezewa thamani soko litakuwepo
tungependa wafugaji wazalishe maziwa ambayo wataweza kuuza.” Amesema Prof.
Gabriel
Ameongeza kuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inatengeneza mazingira
wezeshi kwa wawekezaji ili soko la maziwa liendelee kuwepo kwa kuwa kwa sasa
Tanzania inazalisha maziwa lita Bilioni 2.7 kwa mwaka hivyo yanapaswa
kuongezewa thamani ili kukuza zaidi soko la maziwa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa shirika la SFSI ambalo lipo chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Bahari ya
Jamhuri ya Ireland Bw. David Butler, amesema shirika hilo ilimekuwa likifanya
kazi katika nchini mbalimbali, ambapo limekuwa likifanya vizuri katika sekta ya
nyama na maziwa kwa zaidi ya miaka 40 na kuendesha programu mbalimbali za
kilimo na mifugo ili kuyaongezea thamani mazao.
Bw. Butler ameambatana na
Dkt. Seamus Crosse kutoka Shirika la Greenfield International la Jamhuri ya Ireland,
ambapo wawekezaji hao watakutana na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo
na Uvuvi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ili kuangalia namna ya bora ya
uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni