TANZANIA NA UGANDA ZASAINI MAKUBALIANO YA KUBORESHA SEKTA YA MIFUGO Na John Mapepele Tanzania na Uganda leo zimesaini makubaliano ya kuboresha sekta ya mifugo baina ya nchi mbili kwa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kuthibiti magonjwa hatari ya mlipuko na kuanzisha minada ya pamoja ya kimataifa kwa maslahi ya nchi zote mbili. Makubaliano hayo yamesainiwa kwa upande wa Uganda na Balozi wa Uganda nchini bwana Richard Tumusiime Kabonero na kwa upande wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo mjini Bukoba. Akizungumza mara baada ya utiaji wa saini makubaliano hayo Balozi Kabonero amesema magonjwa ya mlipuko kwa wanyama hayana mipaka hivyo makubaliano yaliyofanyika yatasaidia kudhibiti magonjwa ya wanyama hatimaye kuboresha mifugo. Aidha, amesema hatua ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo itasaidia kupata mifugo bora itakayokuwa na thamani kubwa katika masoko y...