Nav bar

Jumatano, 20 Desemba 2017


Tanzania na Uganda yapiga hatua katika kudhibiti magonjwa ya milipuko


Na John Mapepele
Balozi wa Uganda nchini Bw Richard Tumusiime Kabonero amesema ushirikiano wa karibu baina ya Tanzania na Uganda kwenye sekta ya mifugo unahitajika ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko ambayo ni hatari kwa mifugo ya pande zote mbili.
Akizungumza leo mjini Bukoba kwenye mkutano wa wataalam wa mifugo wa Tanzania na Uganda ulioandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini, Balozi Kabonero amesema njia bora ya kudhibiti magonjwa ya wanyama ni kuwa na timu ya pamoja ya wataalam watakaokuwa wakifuatilia hali ya mifugo na kufanya tathmini kila wakati badala ya utaratibu wa sasa wa kila nchi kushughulikia peke yake.
“Uganda kama ndugu wa karibu wa Tanzania tuna kila sababu ya kushirikiana ili kuboresha sekta hii” alisisitiza balozi Kabonero
Akizungumzia kwa upande wa Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo amewataka wafugaji wa asili kote nchini wabadili mitazamo ya kutegemea serikali katika kukuza sekta badala yake washirikiane nayo ili kuharakisha mapinduzi ya sekta ya mifugo.
“Bado kuna kazi ya kubwa ya kufanya ili kuikwamua sekta, lakini pia tukiamua kwa pamoja baina ya serikali na wafugaji nadhani tutakuwa na kipindi kifupi tu cha kufanya mabadiliko makubwa kwenye sekta hii” aliongeza Dkt. Mashingo
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, bwana Victor Mwita anasema kuwa kuimarika kwa minada itakayosimamiwa kisheria katika mipaka ya nchi ya Tanzania na Uganda itasaidia kuongeza tija katika sekta ya mifugo hapa nchini.
Aidha, Dkt. Mashingo alisisitiza kwamba wafugaji wenyewe ndiyo wanaoweza kuifanya sekta kupiga hatua kwa kuzingatia na kusimamia sheria mbalimbali za mifugo nchini. Alizitaja baadhi ya sheria ambazo ni kipaombele kwa wafugaji kuzingatia kwa sasa kuwa ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo namba 17 ya mwaka 2003 na Sheria za Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo namba 13 ya mwaka 2010.
Akitolea mfano wa mafanikio yaliyoletwa na wafugaji wenyewe nchini , Dkt. Mashingo alisema wafugaji wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa wakati huo marehemu Joel Bendera waliweza kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro iliyokuwepo baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Aidha alisema magonjwa kama Ndigana kali (ECF ) kama ikitokomezwa kabisa yasaidia kuongeza idadi ya mifugo nchini kwa kuwa ugonjwa huo ukiingia unachangia kuua 80% ya ndama wanaozaliwa.
Akichangia katika kikao hicho Mtendaji Mkuu wa Ranchi za Mifugo nchini(NARCO) Profesa Philemoni Wambura alisema bado kuna mahitaji makubwa ya mifugo katika viwanda vya nyama.
“Mahitaji halisi ya ng’ombe wa kuchinjwa katika viwanda vyetu nchini ni 800 kwa siku lakini bado hatujaweza kufikia lengo hilo. Tuna kazi ya kufanya “ alisisitiza Profesa Wambura
Kaimu Mkurugenzi Idara za Huduma za Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Martin Ruheta amesema ili sekta ya mifugo ifanikiwe lazima uzalishaji wa malisho uboreshwe malisho yanachangia kwa asilimia 70 hadi 80 kwa ng’ombe wa maziwa na kwa ng’ombe wa nyama inakwenda mpaka asilmia 90 Katika uzalishaji wa mifugo, hakuna miujiza mingine na ndo maana nchi za wenzetu kama vile Brazil wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta hii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni