Nav bar

Alhamisi, 7 Desemba 2017


 MPINA AMSIMAMISHA KAZI MTUMISHI ALIYESHIRIKI UTOROSHAJI WA KILO 2500 ZA SAMAKI KWENDA BURUNDI ZENYE THAMANI YA SHILINGI 20,850,000.00

Na  John Mapepele

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana  Budeba kumsimamisha  kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana  Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.

Akizungumza katika Ofisi ya Kitengo hicho iliyopo mjini Kagera, Mpina  alisema  mnamo tarehe 03/12/2017 majira ya Saa 03:00  asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.

“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na  barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara moja.” Alisisitiza Mpina

Aidha, Waziri Mpina alisema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo bwana Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo,  na kuongeza kwamba samaki hawa walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.

Afisa Mfawidhi wa Kanda wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina baadhi ya taratibu zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa kwa kuwa  walikuwa wakubwa zaidi ya sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50, msafirishaji kutokuwa na kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi, kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa na cheti cha afya pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.

Waziri Mpina  alisema samaki hao walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha Jeshi la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba pamoja na Shule ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha Mahakama.

Alisema  kazi hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngara. Luteni kanali,Michael Mtenjele. Aliongeza kuwa uchunguzi wa awali ilibaini kuwa samaki hao walitokea kwenye kijiji cha Izigo wilayani Muleba.

Ametaja baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni pamoja na  kukamatwa kwa furu kilo 9100 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa na kuuzwa kwa amri ya mahakama na watuhumiwa wawili kufikishwa mahakamani.

Kukamatwa  kwa uduvi kilo 5000 ambazo zililipiwa mrabaha na mtuhumiwa kulipa faini ya shilingi 100,000/=,kukamatwa  kwa mafurushi 6 ya Samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 katika kituo cha basi cha Kagera zilizotoka mkoani Kigoma kwenda Uganda ambapo mtuhumiwa alikimbia na samaki hao kutaifishwa.

Katika tukio jingine jumla ya kilo 100 za mabondo mabichi ya samaki yamekamatwa kwenye doria mpakani Mtukula na mtuhumiwa  amefikishwa polisi kwa hatua za kisheria.

Waziri Mpina amewaomba wavuvi kuzingatia Sheria na taratibu mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo iwe na tija na kuchangia  katika  uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Wakichangia kwa nyakati tofauti watumishi wa kituo hicho waliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mpina kuangalia namna ya kuongeza nguvu kazi na vitendea kazi mbalimbali vitakavyosaidia kudhibiti uvuvi haramu.

Nahodha Mkuu wa kituo hicho, bwana Ernest Maguzu alisema kazi ya doria katika Ziwa Viktoria imekuwa ngumu kutokana na  maendeleo  makubwa  ya teknolojia ya mawasiliano kwa kuwa wavuvi wamekuwa wakiwasiliana mara moja kutumia simu za mikononi pindi wanapoziona boti za doria zinaingia ziwani na kufanikiwa kukimbia.

Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora na Masoko bi, Theresia Temu aliomba kuongeza udhibiti wa usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na mazao ya uvuvi nje ya nchi kwa kuwa hivi sasa Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na wafanyabiashara kutorosha mazao hayo mipakani bila kulipa ushuru.

Bi Temu alisema kuwa inakadiriwa kuwa zaidi ya tani mia moja ya  mazao ya uvuvi yanatoroshwa kila mwezi katika mipaka ya nchi jirani hivyo jitihada za pamoja baina ya wadau mbalimbali zinahitajika ili kupambana na tatizo hili

“Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo kubwa tunaomba Serikali kuliangalia kwa jicho la tatu namna nyingine tutaendelea kuibiwa” alisisitiza bi Temu

Waziri Mpina  alisema Halimashauri zote nchini zinatakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinza raslimali za majini  na baharini kwa kuwa  licha ya  raslimali hizo kutoa mchango  mkubwa wa uchumi kwa taifa pia manufaa yake ni kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.

“Nataka suala la uvuvi wa mabomu na nyavu za kukokota liwe historia katika nchi yetu. Tutaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote  atakaje tuhujumu” alisisitiza Mpina


 Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Mhe.Luhaga Mpina  akiangalia  maboksi ya samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 yaliyokamatwa katika kituo kikuu cha basi cha  mjini Kagera hapo jana
Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Mhe.Luhaga Mpina akitoa  tamko la kumsimamisha  kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana  Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/=

Moja ya boti inayotumika kwenye doria katika ziwa Viktoria na  Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni