Na John Mapepele
Tanzania na Uganda leo zimesaini makubaliano ya kuboresha sekta ya mifugo baina ya nchi mbili kwa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kuthibiti magonjwa hatari ya mlipuko na kuanzisha minada ya pamoja ya kimataifa kwa maslahi ya nchi zote mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa kwa upande wa Uganda na Balozi wa Uganda nchini bwana Richard Tumusiime Kabonero na kwa upande wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo mjini Bukoba.
Akizungumza mara baada ya utiaji wa saini makubaliano hayo Balozi Kabonero amesema magonjwa ya mlipuko kwa wanyama hayana mipaka hivyo makubaliano yaliyofanyika yatasaidia kudhibiti magonjwa ya wanyama hatimaye kuboresha mifugo.
Aidha, amesema hatua ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo itasaidia kupata mifugo bora itakayokuwa na thamani kubwa katika masoko ya kimataifa na kuingizia nchi zote mbili mapato zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo nchi zinapata hasara kwa kuuza mifugo ikiwa katika kiwango cha chini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo amesisitiza kwamba ushirikiano wa kitaalam katika kuratibu,kufuatilia hali ya mifugo na kufanya tathmini ya kila wakati utaleta mafanikio makubwa baina ya nchi ya Tanzania na Uganda utaleta mapinduzi katika sekta badala ya utaratibu wa sasa wa kila nchi kushughulikia masuala ya peke yake.
“Magonjwa ya mlipuko kwa wanyama ni suala mtambuka duniani kote, hivyo ni muhimu kulishughulikia kwa pamoja ili kuwa na tija” alisisitiza Dkt. Mashingo.
Kwa upande wa himasheria, Dkt. Mashingo amesema kuwa serikali zote zimeangalia namna bora ya kushirikiana utekelezaji wa sheria ili kuwabana wafugaji wasiozingatia sheria kwenye sekta hiyo.
“Tumeamua kwa pamoja kuanzia sasa kudhibiti tatizo la utoroshaji wa mifugo kwenye mipaka ya nchi zetu. Hatua kali zitachukuliwa ili kutoa fundisho kwa yeyote atakayefanya makosa”
Amesema ili kuboresha masoko ya mifugo baina ya Uganda na Tanzania wamekubaliana kuwa na minada ya kimataifa katika maeneo ya Mutukula kwa upande wa Tanzania na Kamwema kwa upande wa Uganda.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, bwana Victor Mwita anasema kuwa kuimarika kwa minada itakayosimamiwa kisheria katika mipaka ya nchi ya Tanzania na Uganda itasaidia kuongeza tija katika sekta ya mifugo hapa nchini.
Aidha, Dkt. Mashingo alisisitiza kwamba wafugaji wenyewe ndiyo wanaoweza kuifanya sekta kupiga hatua kwa kuzingatia na kusimamia sheria mbalimbali za mifugo nchini. Alizitaja baadhi ya sheria ambazo ni kipaombele kwa wafugaji kuzingatia kwa sasa kuwa ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo namba 17 ya mwaka 2003 na Sheria za Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo namba 13 ya mwaka 2010.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni