WATAALAM WA MIFUGO WANA FURSA KUBWA KUINUA SEKTA KUPITIA C-SDTP

Na Chiku Makwai; Mbeya

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele, amesema wataalam wanaopatiwa mafunzo kupitia Mradi wa Mageuzi ya Sekta ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) wana nafasi kubwa ya kuchochea mageuzi na kuinua sekta ya mifugo nchini.

Dkt. Madele ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2026, katika Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Uyole, mkoani Mbeya, wakati akizindua Mafunzo ya Wawezeshaji wa Mashamba Darasa ya Ng’ombe wa Maziwa yanayotekelezwa kupitia mradi wa C-SDTP, amesisitiza  kuwa wataalam wanapaswa kuhakikisha maarifa na teknolojia wanazozitoa zinaendana na mazingira uwezo wa mfugaji pamoja na rasilimali zinazopatikana katika eneo husika.

“Kutibu mifugo siyo sifa nzuri pekee kwa mtaalam; sifa kubwa ni kuzuia magonjwa ya mifugo ili kuhakikisha tunapata maziwa bora na salama yenye viwango vinavyokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Madele.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea wataalam uwezo wa kubaini aina na mifugo inayofaa kulingana na mazingira ya mfugaji, pamoja na kuimarisha matumizi ya lishe bora ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene, amesema LITA imepewa jukumu la kuendesha mafunzo kwa wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa kupitia mfumo wa Shamba Darasa, unaowezesha wafugaji kujifunza kwa vitendo kwa kushirikiana katika vikundi.

Amesema mfumo huo unawapa wafugaji fursa ya kutambua changamoto zinazowakabili, kuchagua suluhisho, kufanya majaribio na kutathmini matokeo kwa lengo la kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato.

Naye Mtaalam wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira wa C-SDTP, akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Mradi, Ndg. Joseph Kihaule, ameipongeza LITA kwa kasi nzuri ya utekelezaji wa mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu madhubuti wa kuwafuatilia wataalam baada ya kumaliza mafunzo, ili kuhakikisha maarifa wanayopata yanawafikia wafugaji na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Lita Dkt. Pius Mwambane akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wawezeshaji wa shamba darasa ya Ng’ombe wa maziwa kupitia C-SDTP uliofanyika Oktoba 5, 2026 Mati Uyole mkoani Mbeya.

Mtaalam wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira wa C-SDTP, akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Mradi, Ndg. Joseph Kihaule akichangia jambo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wawezeshaji wa shamba darasa ya Ng’ombe wa maziwa kupitia C-SDTP uliofanyika Oktoba 5, 2026 Mati Uyole mkoani Mbeya.




Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE), Bw. Samwel Mdachi akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wawezeshaji wa shamba darasa ya Ng’ombe wa maziwa kupitia C-SDTP uliofanyika Oktoba 5, 2026 Mati Uyole mkoani Mbeya.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI