TVLA YATOA ELIMU YA AFYA YA MIFUGO KATIKA MAONESHO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI MUFINDI
Na. Daudi Nyingo
WAKALA ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imetoa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala, ikiwemo uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo, matumizi sahihi ya chanjo na uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, kwa wananchi na wadau wanaotembelea Maonesho ya Biashara na Uwekezaji ya Wilaya ya Mufindi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Wambi, Mafinga Mjini, mkoani Iringa.
TVLA inashiriki katika maonesho hayo ya siku nane, yanayofanyika kuanzia Oktoba 16 hadi 23, 2026, kupitia Kituo chake cha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kilichopo Iringa, kinachohudumia mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya, ambapo imeweka banda maalumu na kupeleka wataalamu kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na Wakala.
Ushiriki wa TVLA katika maonesho hayo unaongozwa na Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dkt. Geofrey Mbata, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Wakala za kusogeza huduma zake karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu afya ya mifugo na kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya mifugo.
Katika banda hilo, wataalamu wa TVLA wanatoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya chanjo za mifugo katika kuzuia magonjwa, ikiwemo kuzingatia ratiba za uchanjaji, matumizi ya chanjo kulingana na aina ya mifugo na magonjwa yanayokingwa, pamoja na uhifadhi sahihi wa chanjo ili kudumisha ubora na ufanisi wake.
Aidha, wataalamu hao wanatoa elimu kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa magonjwa ya mifugo katika maabara kwa ajili ya kupata utambuzi sahihi, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, udhibiti wa ubora wa viuatilifu pamoja na huduma nyingine za kitaalamu zinazotolewa na TVLA kwa lengo la kuboresha afya ya mifugo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Kupitia maonesho hayo, TVLA inaendelea kutumia fursa ya kukutana na wafugaji, wafanyabiashara na wadau mbalimbali ili kutangaza bidhaa na huduma zake, kuongeza uelewa wa wananchi na kupanua wigo wa masoko ya huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini.
Maonesho hayo ya Biashara na Uwekezaji ya Wilaya ya Mufindi yamewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji, kuimarisha ushirikiano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.





Maoni
Chapisha Maoni