TVLA YAPELEKA ELIMU YA AFYA NA LISHE YA KUKU TANZANIA POULTRY SHOW 2026
Na. Daudi Nyingo – Dar es Salaam
WAKALA ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imetoa elimu kuhusu huduma inazozitoa hasa katika kinga na uchunguzi wa magonjwa pamoja na uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo kwa wadau waliohudhuria Maonesho ya 10 ya Kuku na Ndege Wafugwao (Tanzania Poultry Show 2026). Maonesho hayo yamefanyika Oktoba 16–17, 2026, Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, huku elimu hiyo ikilenga kuwasaidia wafugaji kulinda afya ya kuku na kuongeza tija.
Akizungumza Oktoba 17, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyama wa TVLA, Dkt. Scholastica Doto, amesema kwa wadau waliotembelea banda wameelimishwa uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo, uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, usajili na udhibiti wa viuatilifu vya mifugo pamoja nautafiti wa magonjwa ya wanyama
“Tumetumia maonesho haya kuwafikishia wadau waliotembelea banda letu elimu kuhusu huduma za TVLA na namna zinavyoweza kuwasaidia katika ufugaji. Tunataka mfugaji afahamu mahali pa kupata uchunguzi wa magonjwa, chanjo na uhakiki wa chakula, ili afanye maamuzi kwa ushauri wa kitaalamu na kulinda uwekezaji wake,” amesema Dkt. Doto.
Miongoni mwa elimu iliyotolewa ni matumizi sahihi ya TEMEVAC, chanjo inayozalishwa na TVLA kwa ajili ya kukinga kuku dhidi ya kideri, unaojulikana pia kama mdondo ambapo wadau wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya uhifadhi, usafirishaji na uchanjaji ili chanjo itumike ipasavyo.
Akizungumzia uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, Afisa Utafiti wa Mifugo wa TVLA, Fredrick Mwakaje, amesema elimu iliyotolewa inalenga kumsaidia mfugaji kufahamu ubora wa chakula anachotumia na kumpa mzalishaji taarifa za kuboresha bidhaa zake. Ameeleza kuwa TVLA huchambua virutubishi, ikiwemo protini, nishati na madini, pamoja na ubora wa malighafi zinazotumika kutengeneza vyakula vya mifugo.
Baadhi ya wadau waliotembelea banda la TVLA wamefurahishwa na elimu kuhusu uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo na matumizi sahihi ya chanjo ya TEMEVAC, wakieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia katika kulinda afya za mifugo yao hasa kuku na wameahidi kutumia huduma za maabara kuhakiki ubora wa chakula, kuzingatia maelekezo ya uhifadhi, usafirishaji na utoaji wa chanjo, pamoja na kutafuta ushauri wa kitaalamu katika shughuli zao za ufugaji.





Maoni
Chapisha Maoni