TDB YAZIDI KUSIMAMIA UBORA WA MAZIWA, YAFANYA UKAGUZI NZUGUNI NA KISASA
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) leo Oktoba 06, 2026 imefanya ukaguzi wa kawaida wa maziwa na bidhaa zake katika Kata za Nzuguni na Kisasa, jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi viwango vya ubora na usalama kwa walaji.
Ukaguzi huo uliongozwa na Mtekinolojia wa Chakula, Bw. John Isaay, ambaye amewasisitiza wafanyabiashara wa maziwa wa madukani kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zinazowekwa na TDB, ikiwemo kuhakikisha biashara zao zinaendeshwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.
Bw. Isaay amesema uzingatiaji wa taratibu hizo ni muhimu katika kulinda afya za walaji na kuhakikisha maziwa yanayouzwa kwa wananchi yanakuwa salama na yenye ubora unaokubalika.
Amesema TDB itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuongeza uelewa kuhusu wajibu wao na kuimarisha uzingatiaji wa viwango katika Tasnia ya Maziwa.
Ukaguzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la TDB la kusimamia Tasnia ya Maziwa na kuhakikisha wananchi wanapata maziwa na bidhaa zake zilizo salama na zenye ubora.



Maoni
Chapisha Maoni