TASFAM KUELEKEA SENSA YA UVUVI KIDIJITALI 2026

Na. Edward Kondela

Imeelezwa kuwa zoezi la kutathmini Sensa ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Mwaka 2026 kwa njia ya kidijitali, limefika katika muda muafaka kwa kuachana na mambo ya kizamani na kuingia kwenye mfumo unaotambulika kimataifa.

Hayo yameelezwa leo (15.10.2026) na Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Kanda ya Deep Sea katika Halmashauri ya Jiji la Tanga Bw. Bahero Adhio Salim, wakati baadhi ya viongozi wa chama hicho na wavuvi wakitaarifiwa na wasimamizi wa sensa na wakusanya takwimu, juu ya ujio wa sensa hiyo itakayofanywa mwezi huu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mradi wa Kukuza Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Bahari Tanzania (TASFAM).

Kuhusu sensa hiyo itakayofanyika kwa mfumo wa FAIMS na jinsi ya kukusanya takwimu kwa kuhusisha mialo yote ya uvuvi iliyopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi katika mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, Bw. Salim amesema wana matarajio itakuwa na matokeo chanya katika kufahamu idadi ya wavuvi na shughuli wanazofanya.

“Nitawashauri na kuwaeleza wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali halikadhalika zoezi hili litakuwa pia na tija katika upande wa uhifadhi wa mazingira.” amesema Bw. Salim

Naye, Afisa Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga Bw. Ezra Katete, amesema wamefanya mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya maandalizi ya  Sensa ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Mwaka 2026, ambapo zoezi hilo ni muhimu kwa kutoa matokeo ya takwimu mbalimbali ambazo zitasaidia katika kutengeneza sera na miongozo inayosimamia shughuli za uvuvi.

Ameongeza kuwa kila mdau ashiriki kikamilifu ili kupata takwimu sahihi na kwamba watafanya kazi kwa nguvu zote ili takwimu zipatikane na kuwaomba watakaokuwa wadadidi wajitahidi kukusanya takwimu sahihi pamoja na taarifa zote zinazohitajika ili sera na miongozo mbalimbali itakapotengezwa kwa kutumia takwimu itakayopatikana kuwezesha kusimamia shughuli za uvuvi.

Zoezi la sensa linafanyika katika hatua mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa sensa na wakusanya takwimu ambapo zoezi hili limezinduliwa rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani na kutolewa mafunzo kuanzia tarehe 05 hadi 07 Oktoba 2026 na linaratibiwa na timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.  

Kwa sasa mafunzo yanatolewa wasimamizi wa sensa na wakusanya takwimu kwenye maeneo yote ya mialo na yanahusisha usajili wa wadadisi wa sensa katika Mfumo wa FAIMS na jinsi ya kukusanya takwimu.

Baada ya mafunzo ya wadadisi kukamilika timu ya wizara kwa kushirikiana na maafisa wa Halmashauri itaendesha zoezi la sensa ya uvuvi.

Kaulimbiu ya zoezi hili ni "Takwimu Sahihi za Uvuvi, Msingi wa Uvuvi Endelevu Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.







Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI