TANZANIA YAKABIDHIWA UENYEKITI WA BARAZA LA MAWAZIRI WA UVUVI AFRIKA MASHARIKI

Bujumbura, Burundi

Tanzania imekabidhiwa Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji Afrika Mashariki (FASCoM), katika Mkutano wa Nane wa Kawaida wa Baraza hilo uliofanyika Oktoba 6, 2026, jijini Bujumbura, Burundi, chini ya Taasisi ya Usimamizi wa Uvuvi Ziwa Victoria (LVFO).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, amesema Tanzania itahakikisha maamuzi, maazimio, mikakati na mipango ya kikanda inayolenga kuendeleza na kusimamia rasilimali za uvuvi na ukuzaji viumbemaji inatekelezwa kwa ufanisi.

Aidha, Mhe. Kamani amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi wanachama katika kusimamia rasilimali za maji zinazovuka mipaka, na amesema kuwa Ziwa Victoria ni rasilimali ya pamoja inayohitaji usimamizi wa pamoja, hasa katika kukabiliana na uvuvi haramu na changamoto ya kupungua kwa samaki. 

Mkutano huo uliwakutanisha Mawaziri na ujumbe kutoka Tanzania, Burundi, Kenya na Uganda, ambazo ni nchi wanachama wa LVFO, na kabla ya kikao cha Mawaziri, Maafisa Waandamizi walikutana kuanzia Oktoba 2 hadi 4, 2026, kujadili masuala ya kitaalamu, kisera na utekelezaji wa maamuzi ya vikao vilivyopita. 

Na baadae kilifuatiwa na kikao cha Kamati ya Uratibu ambacho kilifanyika Oktoba 5, kabla ya masuala hayo kuwasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa ajili ya maamuzi, na miongoni mwa ajenda kubwa zilizojadiliwa ni hatua za kukabiliana na uvuvi haramu, biashara ya samaki wasiokidhi ukubwa unaoruhusiwa na kupungua kwa rasilimali za samaki.

Nchi wanachama zimekubaliana kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha shughuli za uvuvi, uchakataji na biashara ya samaki zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu, na kwa upande wa ukuzaji viumbemaji, mkutano huo umeangazia umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa samaki kwa njia endelevu, kuimarisha usalama wa chakula, ajira na kipato, pamoja na kupunguza shinikizo dhidi ya samaki wa porini, na Tanzania sasa inatarajiwa kuratibu ajenda hizo katika kipindi chake cha uenyekiti.

Uenyekiti huo unaipa Tanzania nafasi ya kuongoza ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa rasilimali za maji, udhibiti wa uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi, utafiti, matumizi ya takwimu za kisayansi na maendeleo ya ukuzaji viumbemaji, hatua ambayo inalenga kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinatumika kwa njia endelevu na kuchangia usalama wa chakula, ajira, biashara, kipato na maendeleo ya wananchi wa Afrika Mashariki.








Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI