SIKU YA CHAKULA DUNIANI: MAPINDUZI USALAMA WA CHAKULA, LISHE BORA

◼️Bodi ya Maziwa vinara wa jumla Taasisi za Serikali

Siku 7 za Maadhimisho ya Wiki ya Chakula duniani yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga zimehitimishwa rasmi leo Oktoba 16,2026 huku simulizi isiyofutika vichwani mwa wengi ikiwa ni mtindo wa hamasa ya vyakula vya protini itokanayo na wanyama na samaki iliyofanywa na 

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi zake.

Katika hotuba yake ya kuhitimisha Maadhimisho hayo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Batilda Buriani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewaasa wakulima, wafugaji na wavuvi kuendelea kuzalisha mazao yanayopewa kipaunbele upande wa lishe na kuzingatia ushauri na maelekezo ya wataalam ili kuwa na uzalishaji endelevu na kuepuka upotevu wa mazao.

“Lengo la Maadhimisho haya mbali na kuboresha afya ya jamii ni kujenga uelewa kuhusu uzalishaji na matumizi ya makundi mbalimbali ya vyakula, matumizi ya pembejeo na mbinu bora za shughuli za ugani”  Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Kwa upande wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa nchini (FAO) Bi. Tipo Nyabenyi mbali na kuipongeza Serikali kwa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi mazingira wezeshi  amebainisha kuwa siku ya Chakula Duniani sio tu inakumbusha jamii juu ya matumizi ya mlo uliokamilika bali inahamsisha ubunifu unaojumuisha teknolojia za kisasa za uzalishaji na ujuzi wa ndani unaokubalika na jamii yote na usiomuacha yoyote nyuma.

Katika Maadhimisho hayo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) ilitoa kiasi cha kilo 130 za samaki aina ya Jodari na kilo 120 za nyama ambazo ziliandaliwa na kupikwa katika mitindo tofauti na kugawiwa kwa wananchi wote waliohudhuria kwenye viwanja vya Usagara huku Bodi ya Maziwa ikiandaa jumla ya pakiti 2400 za maziwa na kuzigawa kwa wananchi na shule 8 za Msingi zilizopo mkoani humo.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI