SERIKALI: SEKTA ZA UZALISHAJI ZIKISHIRIKIANA ZITASAIDIA KUTEKELEZA DIRA 2050
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema serikali imeendelea kuhimiza juu ya umuhimu wa kufungamanisha sekta za uzalishaji ili kuongeza tija kwa wazalishaji wadogo, wa kati na Wakubwa hatua itakayoimarisha sekta hizo na kukuza uchumi wa nchi pamoja na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameitoa Kauli hiyo leo Oktoba 16, 2026 Jijini Dodoma wakati alipomtembelea mjasiriamali mdogo anayefuga Samaki kwa Teknolojia ya Mabwawa, pamoja Ufugaji wa ng'ombe wa Maziwa na Kuku.
Amesema Sekta za uzalishaji zikifungamanishwa na kusimamiwa pamoja zinamchango mkubwa katika kuongeza tija, akitolea mfano jinsi sekta ya mifugo na uvuvi, kwa mjasiriamali huyo zilivyofanikiwa kupitia sekta zingine ikiwemo Maji, Fedha, Kilimo na Nishati hatua ambayo imemrahisishia mjasiriamali huyo kufanya uwekezaji wenye Tija.
Aidha, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru alieleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, itaendelea kushirikiana na kuziwezesha sekta binfasi na wawekezaji wadogo wakiwemo wanawake na vijana ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 ya kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachangia zaidi asilimia 70 katika uchumi wa taifa.
Awali Mwekezaji na Mfugaji wa Mifugo na Samaki Jijini Dodoma Bi. Carlorine Shio alieleza kuwa mahitaji ya maziwa mkoani humo ni makubwa ukilinganisha na uzalishaji wake ambapo kwa sasa anazalisha na kuuza lita 200 kwa siku, huku mpango wake ni kupanua wigo wa uwekezaji ili kuyafikia masoko makubwa zaidi ya bidhaa za mifugo na uvuvi.









Maoni
Chapisha Maoni