SERIKALI KUTOZA ADA ZA UVUVI KWA SHILINGI, YAPANGA KUSOGEZA HUDUMA ZA VIBALI KWA WANANCHI

Serikali imeanza kutekeleza utaratibu wa kutoza ada na tozo za uvuvi kwa kutumia shilingi za Kitanzania badala ya dola za Marekani, huku ikiahidi kutafuta njia za kusogeza huduma za vibali vya kusafirisha mazao ya uvuvi karibu na wananchi, hatua ambayo inalenga kuwawekea mazingira rafiki wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi nchini.

Akijibu maswali ya Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, Mhe. Moses Ludovico Kaegele leo Oktoba 27, 2026 Bungeni Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, amesema maboresho ya kanuni za ada na tozo za uvuvi yamechapishwa katika Gazeti la Serikali lenye GN Na. 158J la Juni 30, 2026, na kuanza kutumika rasmi julai mwaka huu, na ameweka wazi kuwa mabadiliko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kutumia shilingi za Kitanzania katika ulipaji wa ada na tozo.

Aidha, Mhe. Kamani ameeleza kuwa Wizara itatoa maelekezo kwa maafisa wa uvuvi nchini kote kuhakikisha ada na tozo zinazohusika zinalipwa kwa shilingi kama zilivyoainishwa kwenye kanuni, bila kutegemea kupanda au kushuka kwa thamani ya dola ya Marekani, na amesema utaratibu huo unalenga kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi na biashara ya mazao yake.

Katika swali lake la pili, Mhe. Kaegele aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwajengea uwezo watendaji wa vijiji ili waweze kusaidia kutoa vibali vya kusafirisha mazao ya uvuvi, akieleza kuwa baadhi ya wavuvi hulazimika kufuata huduma hizo katika maeneo ya mbali, akijibu hoja hiyo, Mhe. Kamani amesema vibali hivyo hutolewa kupitia mfumo wa kielektroniki wa FiRCIS, unaotumiwa na maafisa 46 nchini wenye uwezo wa kutoa namba za malipo (Control Number) na vibali.

Vilevile, Mhe. Kamani amekiri kuwa idadi ya maafisa hao bado haitoshelezi mahitaji na kusema Serikali inaendelea kuajiri kulingana na upatikanaji wa fedha na mipango yake, na kuhusu pendekezo la kuwajengea uwezo watendaji wa vijiji, amesema Wizara imelipokea na itafanya utafiti kubaini namna bora ya kusogeza huduma hizo karibu na wananchi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo, hatua inayolenga kupunguza usumbufu na kurahisisha shughuli za wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI